|
Nitawaita Ivo, Nsajigwa - Maximo
2008-04-25 09:29:32
By Somoe Ng\'itu
Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo jana alitangaza kikosi cha wachezaji watakaojiandaa na mechi dhidi ya Uganda, The Cranes na kusema kuwa bado anasubiri hatma ya adhabu ya aliyekuwa kipa wake namba moja, Ivo Mapunda na beki, Shadrack Nsajigwa.
Wachezaji hao ndio pia watajiandaa na mechi za kuwania kufuzu kucheza fainali za mashindano ya Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika zilizopangwa kufanyika mwaka 2010.
Maximo alisema kuwa anaheshimu maamuzi ya kuwasimamisha wachezaji, Ivo na Nsajigwa ambayo yalitolewa na uongozi wa Yanga na licha ya kuwahitaji lakini atatangaza kuwaongeza wachezaji hao endapo klabu hiyo itakuwa imetoa maamuzi ya kuwarejesha baada ya kumaliza kutumikia adhabu yao ambayo inayomalizika leo.
Maximo alisema kuwa wachezaji aliowaita anaamini kuwa wataendelea kufanya vizuri baada ya kupata mafunzo zaidi hasa wakifahamu kuwa mechi dhidi ya Uganda zinazowakabili ni ngumu.
``Wachezaji sio kama mashine, unapowasha tayari inaanza kufanya kazi, wao wanahitaji kuandaliwa ili kuboresha viwango vyao,`` alisema Maximo.
Aliwataja wachezaji 20 ambao wanajiandaa na mchezo wa Mei 3 kuwa ni pamoja na Farouk Ramadhani, Shabani Dihule, Fred Mbuna, Kelvin Yondan, Nadir Haroub, Salum Sued, Juma JAbu, Amir Maftah, Stephano Mwasyika, Henry Joseph, Shabani Nditi na Athumani Iddi.
Wengine ni Godfrey Bonny, Ulimboka Mwakingwe, Uhuru Suleiman, Abdi Kassim, Mrisho Ngassa, Emmanuel Gabriel, Jerry Tegete na Kigi Makasi.
Aliwataja wachezaji wengine watano ambao wataungana na wenzao kwa ajili ya mechi dhidi ya Mauritius iliyopangwa kufanyika Mei 31 hapa nchini kuwa ni Erasto Nyoni, Meshack Abel, Haruna Moshi, Nizar Khalfan na Danny Mrwanda.
Stars imefanikiwa kusonga mbele katika mashindano hayo mapya yanayoandaliwa na Shirikisho la soka la Afrika (CAF) baada ya kuifunga Kenya, Harambee Stars jumla ya mabao 2-1.
|