|
...Simba yamsimamisha Henry Joseph
2008-04-26 09:04:30
By Onesmo Kapinga
Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umeendeleza tabia yake ya kufungia wachezaji na panga safari hii limemwangukia kiungo mahiri, Henry Joseph, ambaye amesimamishwa kutocheza soka hadi Mei 8, kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.
Hatua hiyo sasa itafanya akose mchezo wa kesho dhidi ya Yanga, ambao ndio utakuwa wa kufunga pazia la ligi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda alisema kuwa mchezaji huyo amefungiwa kutokana na kutoweka bila taarifa wakati timu hiyo ilipocheza na Kagera Sugar, Jumatano wiki hii.
Kaduguda alisema kuwa baada ya kutumikia adhabu yake uongozi wa klabu hiyo, utamwita ili aweze kujieleza kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.
Mchezaji huyo, amefungiwa ikiwa imebakia siku moja kupambana na watani wao wa jadi, Yanga katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.
Hata hivyo, jana uongozi wa klabu uliwafunguliwa wachezaji sita waliofungiwa hivi karibuni kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.
Wachezaji hao ni Athumani Machupa, Victa Costa, Yahaya Akilimali, Nurdin Bakari na Said Sued na Erick Majaliwa.
Wakati huo huo, alisema kuwa timu ya Simba hawahitaji kufanya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Yanga utakaofanyika kesho.
Alisema kuwa katika mchezo huo Yanga kufungwa ni lazima na hilo halina ubishi kwao.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa, Oktoba 24, mwaka jana kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Simba waliibuka na ushindi wa 1-0.
|