|
Waandamana kupinga Nyamagana kubomolewa
2008-04-26 09:05:06
By George Ramadhan, PST Mwanza
Wakazi wa jiji la Mwanza jana jioni waliandamana katika mitaa ya jiji hilo kupinga hatua ya Halmashauri ya Jiji hilo kuamua kuuza uwanja wa Nyamagana kwa wawekezaji.
Wananchi hao walichukua uamuzi huo kufuatia uamuzi wa jiji hilo kutoa uwanja huo kwa wawekezaji ili waweze kuubomoa na kutengeneza vitega uchumi.
Waandamanaji hao walianza kuandamana wakipita katika mitaa mbalimbali wakiwa na mabango yakiwa yamejaa maandishi ya kukashifu viongozi kwa hatua hiyo.
Mathalani bango moja lilisema `Mmeleta makocha kutoka Brazil watafanyisha mazoezi wapi` likiwa na maana wachezaji watapatikana vipi ikiwa uwanja huo utauzwa.
Uwanja huo hutumika kwa ajili ya mechi za mashule na zile za ligi ya mkoa huo.
Hatua hiyo ya jiji, hata hivyo, imepingwa tayari na Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Lawrence Masha, ambaye alieleza uwanja huo haupaswi kuvunjwa kutokana na kuwa wa kihistoria.
Alitoa mfano wakati Baba wa Taifa, Hayati Mwaluimu Julius Nyerere wakati akidai uhuru wa Tanganyika alikuwa akitumia uwanja huo na pia unakumbukwa kutokana na mechi ya Simba na Yanga ya mwaka 1974, ambapo Simba ililala 2-1.
Akizungumza bungeni juzi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliunga mkono uwanja huo kubomolewa lakini alionya kunahitajika ridhaa ya wananchi wa mkoa wa Mwanza.
Akipokea maandamano ya wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. James Msekela aliwataka wananchi hao kujaza fomu maalum zinazotolewa na jiji ili kuonyesha wanapinga mpango huo.
|