|
Wachezaji Simba walia njaa kali
2008-04-26 09:05:56
By Mwandishi Wetu
Wachezaji wa timu ya Simba wamesema kuwa bado kambi yao inaendelea kuzungukwa na tatizo la ukata licha ya kukabiliwa na mechi ngumu dhidi ya watani zao, Yanga ambayo imepangwa kufanyika kesho kwenye uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.
Hata hivyo, wachezaji hao wamesema kuwa hali hiyo haiwakatishi tamaa na wanaahidi kuibuka na ushindi katika mchezo huo ili kuweza kuendeleza heshima yao baada ya kuukosa ubingwa.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wachezaji hao walisema kuwa wanaendelea kufanya mazoezi kama kawaida lakini hakuna kikao chochote ambacho kimefanyika kinachoelezea kuwa watapatiwa fedha.
``Hali ni tofauti na miaka mingine, hakuna viongozi wanaokuja kambini kutueleza juu ya fedha wala ahadi, ni kuhimizana kufanya mazoezi kila siku,`` alisema mmoja wa wachezaji hao ambaye yuko katika kikosi cha kwanza tangu mwaka 2003.
Mchezaji mwingine alisema kuwa mwaka huu umekuwa ni mgumu kwa wachezaji wa Simba na kinachowafanya wajitume ni kuendeleza vipaji vyao ili msimu ujao waweze kutafutwa na timu nyingine.
``Ndio tunatatizo la kutopewa fedha zetu, lakini hii haitasababisha sisi kupoteza ushindi katika mechi hiyo ya Jumapili,`` alisema mmoja wa washambuliaji mahiri wa timu hiyo.
Katika hatua nyingine, Kundi la Friend’s of Simba ambalo huwa mstari wa mbele kuzungumza na wachezaji na kuwapa ahadi endapo itashinda mechi hiyo, mpaka jana mchana ilikuwa haijatuma mwakilishi yoyote kukutana na wachezaji hao.
Akizungumza na Nipashe mmoja wa wanachama hao alisema kuwa umefika wakati wa kuona kuwa wachezaji wanajituma na si kucheza kwa jihad baada ya kuahidiwa kuwa watapatiwa fedha.
``Mpaka leo (jana mchana) hatujaambiana kuchanga fedha kwa ajili ya mechi hiyo, ila tumewaeleza vijana kuwa atakayecheza vibaya ndio utakuwa msimu wake wa mwisho, tunajua Yanga hawawezi kusajili zaidi ya wachezaji wawili kutoka Simba,`` alisema kigogo huyo wa Friend’s of Simba.
Simba ambayo inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa na pointi 41 inatakiwa kushinda mechi hiyo na kuiombea dua mbaya Prisons ipoteze mchezo wake wa mwisho ili iweze kumaliza ligi ikiwa ya pili na kushiriki katika mashindano ya Kombe la Shirikisho mwakani.
|