01 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Uboreshaji maslahi ya wafanyakazi, usalama na vitendea kazi unahitajika
 
2008-05-01 11:21:51
Na Peter Tindwa

Leo, Watanzania wanaungana na wafanyakazi wote duniani kusherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi). Sikukuu ya Mei Mosi husherehekewa duniani kote kila tarehe 1 ya mwezi wa Mei.Makala hii ya Mwandishi Peter Tindwa yafafanua.

Wakati mamia ya maelfu ya Watanzania wakiungana na wafanyakazi wenzao kote duniani kusherehekea Mei Mosi, bado harakati za kuboresha maisha, afya pamoja na usalama kwa wafanyakazi nchini zimekuwa zikiendelea.

Harakati hizi zimekuwa zikijumuisha vyama mbalimbali vya wafanyakazi katika sekta zote za uzalishaji nchini.

``Kilio kikubwa cha wafanyakazi nchini ni juu ya maslahi duni hususan mishahara isiyowiana na upandaji wa gharama za maisha kote nchini,`` anasema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Nestory Ngulla.

TUCTA imependekeza kwamba kima cha chini cha mshahara kwa mfanyakazi katika sekta binafsi kiwe ni Sh. 150,000 kwa mwezi wakati katika sekta ya umma kiwe ni Sh. 315,000 kwa mwezi.

``Viwango vya mishahara vilivyopendekezwa na TUCTA vimezingatia gharama halisi za maisha zilivyo na zinavyopanda nchini,`` Ngulla alisema jijini Dar es Salaam hivi karibuni kufuatia migomo ya wafanyakazi katika baadhi ya sekta binafsi.

Kwa upande wake, serikali imekuwa ikisisitiza kuwa mapato yake bado hayaiwezeshi kulipa viwango vipya vya mishahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma.

``Serikali pamoja na wadau wengine hususan TUCTA tumekuwa tukijadiliana juu ya uwezekano wa kulipa viwango vipya vya mishahara. Lakini bado tunakabiliwa na tatizo la ufanisi katika kazi hasa ule wa kuleta tija ili tuweze kupata mapato mengi na tuweze kulipa mishahara mizuri kwa wafanyakazi ndani ya sekta ya umma,`` Waziri wa Serikali Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, alinukuliwa hivi karibuni akisema.

Vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi wenyewe wamekuwa wakishindwa kuielewa misimamo ya serikali juu ya maamuzi hususan yahusuyo viwango vya mishahara.

Wakati wa sherehe za Mei Mosi, mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete aliwaambia wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kuwa, serikali ilishaunda bodi za kisekta ambazo zilikuwa zikipitia na kutathmini uwezo wa uzalishaji, tija pamoja na mapato katika kila sekta ili hatimaye zipendekeze juu ya hatua za kuboresha maslahi ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na mishahara mipya katika sekta husika.

Hata hivyo, serikali kupitia kwa Waziri wa zamani wa Kazi, Michezo na Maendeleo ya Vijana, Bw. John Chiligati, alivitangaza rasmi viwango vipya vya mishahara kwa wafanyakazi katika sekta zote za binafsi na umma. Viwango ambavyo vilipaswa kuanza kutumika mapema mwaka huu.

Utekelezaji huo wa agizo la serikali uligonga mwamba baada ya baadhi ya waajiri hususan katika sekta binafsi kugoma kulitekeleza.

Waajiri walisisitiza kwamba utekelezaji wa agizo hilo ungelazimisha kufungwa kwa viwanda na makampuni yao kwa kuwa viwango vipya vya mishahara hazikuzingatia tija inayopatikana katika makampuni na viwanda nchini.

Matatizo mengine yanayowakumba wafanyakazi nchini ni pamoja na kutopewa vifaa vya usalama kazini, yaani vitendea kazi vya kutosha.

Vifaa hivyo ni pamoja na buti na vifaa vingine vya kufanyia kazi hasa ndani ya viwanda na mashambani hususan yale yatumiayo dawa za kemikali za kuulia wadudu na magugu.

Ukosefu wa vitendea kazi mahali pa kazi umekuwa ukichangiwa kwa kiwango kikubwa na udhaifu wa kuendesha ukaguzi wa mara kwa mara mahali pa kazi.

Ukaguzi huo hupaswa kufanywa na maafisa kazi wakaguzi kutoka wizara na idara husika kote nchini.

Tatizo jingine ambalo linaelekea kutopatiwa ufumbuzi ni lile la baadhi ya waajiri kutowasilisha michango iliyokatwa katika mishahara ya wafanyakazi wao kwa muda muafaka kwenye mifuko ya ustawi wa jamii.

Mifuko hiyo ni kama vile, Mfuko wa Ustawi wa Jamii wa Taifa (NSSF), Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) na mingine iliyoanzishwa kisheria nchini.

Wanachama wa mifuko hiyo wamekuwa wakisisitiza kuwepo na utaratibu wa kuwagawia gawiwo kila baada ya kipindi fulani.

``Mifuko hii ya ustawi wa jamii inapaswa kuwalipa gawiwo wanachama wao kwa sababu mifuko yote iliyopo nchini imejiingiza katika kuwekeza (biashara) na hivyo, kupata faida. Kwa nini isilipe gawiwo kwa wanachama,?`` alihoji Bi. Thabitha Siwale, katika semina mojawapo iliyofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.

Serikali kupitia Wizara ya Fedha imekuwa ikisisitiza kwamba iwapo mifuko hiyo itaanza kulipa gawiwo kwa wanachama wao. Basi mifuko hiyo itajihatarisha kama siyo kufa kabisa na hivyo, wanachama kukosa mafao yao kwa ujumla.

``Mifuko ya jamii imeanzishwa maalum kwa kuwalipa mafao wanachama wake na si kulipa gawiwo kwa wanachama.

Iwapo gawiwo litaanza kulipwa, upo uwezekano mkubwa wa mifuko hiyo kutoweka kabisa,`` Waziri wa Fedha, Athuman Mkullo, alinukuliwa akisema mjini Dodoma hivi karibuni.

Hata hivyo, wakati Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha sikukuu ya Mei Mosi, juhudi za makusudi zinapaswa kufanywa na pande zote, yaani waajiri na waajiriwa kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi pamoja na mazingira ya kazi.

Uboreshaji huo lazima uzingatie ulipaji wa viwango vya mishahara vyenye uwiano na upandaji wa gharama za maisha, uwasilishaji wa michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya ustawi wa jamii pamoja na ulipaji wa mishahara kwa wakati muafaka ndani ya mwezi husika.

Kwa upande wa wafanyakazi, lazima ikumbukwe kuwa ulipaji wa mishahara bora yenye kuwiana na ukuaji wa gharama za maisha utachangiwa na uongezwaji wa uzalishaji pamoja na tija sehemu za kazi.

Hata hivyo, baadhi ya waajiri waepuke kuchukua kigezo cha ``tija`` kuwa kivuli cha kutowalipa vyema wafanyakazi wao.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.