04 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Nyumba ndogo inapokuwa nyumba kubwa!
 
2008-05-04 10:30:20
Na Anti Flora Wingia

Itakumbukwa kwamba wiki iliyopita nilichambua kidogo kuhusu hoja iliyotolewa bungeni kwamba wapo kinababa wanaopigwa na wake zao lakini wanamezea. Huu ni unyanyasaji ambao umejificha lakini wenye maumivu makali kwa wenzetu.

Hilo si jambo jema na yafaa kinamama wenye kijitabia hicho waache mara moja. La sivyo, wenzi wao hao wakiwabadilikia, watafute kwa kujificha.

Na si ajabu ndiyo sababu kinababa wengine huamua kutafuta nyumba ndogo kujiliwaza baada ya suluba toka nyumba kubwa.

Wakati bado tukitafakari hilo, hebu msomaji wangu nikupe kisa kingine kinachoonyesha pia jinsi baadhi ya kinababa wananyanyaswa na hizi wanazoziita nyumba ndogo.

Nyumba hizi zipo ambazo huwapa nafuu kinababa lakini zingine ni mzigo.

Hivi majuzi nikiwa nanunua mahitaji katika duka moja, pembeni aliketi mama mmoja anajipatia soda. Punde akachukua simu yake kumpigia mtu fulani.

Kilichotushangaza tuliokuwa eneo lile ni yale matusi aliyokuwa akiyatoa mfululizo mama yule kwa yule aliyekuwa akizungumza naye.

Ingawa ni matusi mazito(sitayataja) lakini kwa jumla nilichogundua ni kwamba mama yule alikuwa hajamuona mzee wake huyo kwa siku mbili.

Katika baadhi ya matamshi yake kwenye simu alimwambia mwenzake huyo kwamba akijua kuzaa pia afuatilie matunzo ya mtoto.

Siku iliyofuata nilipita tena dukani pale na nikamuuliza muuza duka kama anamfahamu mama yule aliyekuwa anamwaga mitusi.

Kijana muuza duka akasema mwanamama yule amezaa na mzee mmoja mwenye familia yake Ilala.

Mzee yule kutokana na kazi yake, huweza kumaliza hata wiki bila kwenda kwenye mji wake mkubwa na ni kutokana na hali hiyo ndipo akaopoa mwanamama huyo na kuzaa naye. Kila siku akimaliza kazi mzee wa watu huishia kwa mke huyo mdogo.

Sasa kisa cha bi-mdogo kuchukia ni kutokana na bwana yule kutoonekana kwa siku mbili. Kumbe alienda kwa mke wake mkubwa lakini bahati mbaya homa ikamshika huko hata kupelekea kulazwa hospitalini.

Wakati bi-mdogo anapiga simu ya kutukana, mzee alikuwa hoi kitandani.

Hata hivyo inasemekana bibie huyo kesho yake alikwenda hadi kwa mke mkubwa kumfuatilia bwana mzee na ndipo alipogundua kuwa kalazwa hospitalini kutokana na homa kali ya Malaria. Ama kweli usiyoyajua ni kama usiku wa kiza.

Mpenzi msomaji, hizi nyumba ndogo ambazo baadhi ya kinababa wanazikumbatia, kwa wengine ni mzigo mkubwa. Wanafanyiwa vitimbwi lakini wanamezea, eti inzi kufia kwenye kidonda ni halali.

Zipo nyumba ndogo ambazo zimewahamisha waume za watu na hata kusababisha ndoa kubomoka. Yaani wapo watu wametunza ndoa kwa miaka mingi lakini inajitokeza nyumba ndogo na kuzivunjilia mbali. Lakini haya yote niseme ni ya kujitakia kwani yanaepukika.

Kinababa wenye tamaa ya nyumba ndogo, wengi wamejionea suluba zake ikiwa ni pamoja na kulazimishwa kutekeleza maamuzi mazito na magumu. Kwa mfano kujenga nyumba, kununua gari au kumfungulia bibie miradi mikubwa.

Waliokumbwa na zali la aina hii wanaelewa ninachosema hapa.

Hata wale wenye uwezo mdogo nao wamejikuta wakitumbukia katika mtego wa kuwa na mke zaidi ya mmoja.

Mtu ana genge la nyanya na mboga mboga. Lakini utashangaa anapata nyumba ndogo baada ya kuhonga vitu vidogo vidogo.

Utakuta msichana wa kazi anatumwa gengeni kwa mahitaji lakini muuza genge anamtamani na kuanzisha mahusiano.

Wapo wasichana wamekimbia ajira zao na kujikuta wakiwekwa kinyumba na wenye miradi kama hiyo ya genge.

Na jamaa huyu akinogewa haraka anasahau nyumba kubwa na kumwaga sera zote kwa bi-mdogo.

Tuache utani nyumba hizi ndogo zinawatesa sana kinababa wenye macho mpepeso. Suluba wanaoipata wanaelewa wenyewe.

Na kibaya zaidi mzunguko wa aina hiyo ndio kwa kiasi kikubwa umechangia maambukizi ya gonjwa hatari la ukimwi.

Haiwezekani mtu ajigawe na kutumikia wake wawili.
Lazima bwana wa aina hii atambue kuwa anapokuwa kwa mke huyu, na kule kwingine nako kuna mambo.

Kwa ujumla mambo mengine kinababa wanajitakia. Unaye mkeo mrembo uliyemchagua mwenyewe na kumuoa kwa ridhaa yako.

Sasa kwanini umpige kisogo na kuanzisha nyumba ndogo? Nyumba hii ikikusulubu utathubutu kulia? Yafaa unyamaze kimya ulilie rohoni.

Ni kweli kwamba wapo wanaoanzisha nyumba ndogo kutokana na sababu za msingi na wakati mwingine kwa makubaliano.

Mfano mama hajabahatika kupata mtoto. Wapo waliojaribu nje ya ndoa na kupata mtoto au watoto kwa maafikiano.

Lakini wapo wengine waliofanya siri na kuzaa nje ya ndoa japokuwa mke mkubwa naye anao watoto. Wapo waliofanya hivi kwa tamaa zao tu za kimwili, wengine kutokana na jeuri zao za pesa au mali walizo nazo.

Wengine wamezihama nyumba zao kubwa na kuhamia nyumba ndogo. Matokeo yake nyumba hiyo ndogo inageuka kuwa nyumba kubwa.

Kama bibie niliyemzungumzia awali katika makala hii, anachoamini ni kwamba yeye ndiye mwenye uzito kuliko bi-mkubwa kwa kuwa bwana amemdhibiti.
Hii si sawa hata kidogo.

Lakini yafaa kinababa wajifunze kutokana na makosa. Wabakie katika miji yao ya awali waachane na miji hii mipya(nyumba ndogo) ambayo imeonyesha matukio mengi ya suluba na manyanyaso.

Hivi mtaendelea kumezea hadi lini? Vunjeni ukimya vinginevyo hakuna atakayewanasua huko mliko ila ni ninyi wenyewe.

Msomaji wangu, mimi naishia hapa nikupe fursa nawe uchangie suala hilo ili sote tuelimishane. Ukiwa tayari usisite kunikandamizia kupitia email ifuatayo:-

fwingia@yahoo.com
Wasalaam.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.