04 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wabadhirifu wamulikwe manispaa zote
 
2008-05-04 10:31:01
Na Mhariri

Ubadhirifu umechangia sana kuzorotesha shughuli na miradi ya maendeleo nchini. Na kibaya zaidi wanaojihusisha na tabia hiyo chafu ni watendaji wetu waliopewa dhamana ya uongozi lakini wanasaliti umma.

Kwa muda mrefu sasa halmashauri zetu nyingi zimekuwa zikilalamikiwa kufuja au kutafuna fedha zinazopelekwa na serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo kama vile ujenzi wa barabara, vituo vya afya, miradi ya maji, ujenzi wa madarasa na kadhalika.

Wananchi wamekuwa wakilalamikia ufujaji wa fedha za miradi unaofanywa na baadhi ya viongozi wasio waadilifu ambao hufikia hatua na kujiona ni miungu watu wasioweza kuguswa na mtu yeyote.

Inafurahisha kuona sasa mamlaka zetu zimeanza kufumbua macho na kusikia vilio vya wananchi kuhusiana na ubadhirifu unaofanywa waziwazi na viongozi wao, huku shughuli za maendeleo zikizidi kudorora.

Mfano mzuri ni hatua ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,(CAG) Bw. Ludovick Utouch ya kubainisha uoza katika Manispaa ya Kinondoni ambako amethibitisha upotevu wa sh.milioni 100 kwenye ununuzi wa matela ya kuzolea taka.

Uthibitisho huo umo katika taarifa ya matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2007 ambayo imesainiwa na CAG.

Upotevu wa fedha hizo ambazo ni kodi za wananchi ulifanyika wakati wa zabuni za ununuzi wa matela 25 kutoka kampuni moja ya mjini Tanga.

Mtuhumiwa wa fedha hizo ni Meya wa Manispaa hiyo, Salum Londa ambaye hata hivyo amekanusha na kutakiwa ajiuzulu, hatua ambayo hajachukua hadi sasa.

Siyo siri kwamba wapo viongozi katika manispaa zetu ambao kazi yao ni kupanga mikakati na mbinu ovu za kutafuna fedha za maendeleo zilizotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Wengi wamekuwa wanajichimbia kwenye eneo la manunuzi ili kutimiza malengo yao ya wizi.
CAG asiishie manispaa ya Kinondoni tu bali azungukie manispaa zingine ambako vilio vya wananchi ni vingi na kwa muda mrefu fedha zimekuwa zikimegwa na wajanja huku miradi ya maendeleo ikodorora au kutekelezwa chini ya viwango kutokana na fedha nyingine kutiwa mifukoni.

Ni muhimu sote tuisaidie serikali kufichua viongozi wabadhirifu wa mali za umma hatimaye tubakie na wale wasafi, waadilifu ambao wana uchungu na maendeleo ya nchi yetu.

Watakaobainika kuhujumu mali na miradi ya wananchi wachukuliwe hatua kali ili liwe fundisho kwa wengine wenye dhamira mbaya.

Huu ni wakati wa viongozi wetu kujitizama na kupima matendo yao na kama wanajielewa siyo wasafi waachie ngazi mara moja.

Vita dhidi ya mafisadi ndio kwanza imeanza na wanaojijua ni wahujumu wajiandae kufungasha virago kwani Serikali ya Awamu ya Nne haimtizami mtu usoni.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.