|
Adhabu zidhibitiwe mashuleni
2008-05-07 08:52:19
Na Mhariri
Madhumuni ya kuwaadhibu wanafunzi wanaopatikana na hatia mashuleni, ni kwa ajili ya kuwaonya ili wajirekebishe.
Lakini, kulingana na matukio yanayozidi kujitokeza kwenye shule mbalimbali nchini, kuna kila sababu ya kuzidhibiti adhabu hizi kufuatia baadhi ya walimu kuzidi mipaka.
Miongoni mwa matukio kama haya, ni hatua ya uongozi wa Shule ya Sekondari ya Kifaru, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro kuamua kuwafukuza wanafunzi zaidi ya 1,200 kutokana na vurugu zilizoanzia kwa wanafunzi kupinga adhabu ya kushika kinyesi cha binadamu.
Imedaiwa kwamba, adhabu hiyo ilitolewa na uongozi wa shule hiyo baada ya mwanafunzi mmoja kudaiwa kujisaidia haja kubwa kwenye korido shuleni hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Bw. Gordian Lugimbana alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama imeunda tume ya madai ya wanafunzi hao kufukuzwa shuleni.
Japokuwa suala hili bado linafanyiwa uchunguzi ili kubaini ukweli, tumekuwa tukishuhudia baadhi ya walimu kuwaadhibu wanafunzi katika hali za kuwadhalilisha au wakati mwingine hata kuhatarisha maisha yao.
Tunafahamu kabisa kwamba endapo mwanafunzi anakosea, mathalani kuwa mtoro, ni lazima aadhibiwe, ilimradi adhabu hiyo itasaidia kumfanya ajirekebishe tabia yake.
Baadhi ya adhabu ambazo tunadhani ni za busara zinaweza kuwa pamoja na kufanya usafi wa mazingira, kutengeneza bustani, kupiga deki madarasa na kadhalika.
Hizi ni adhabu ambazo tunaamini kwamba zinajenga na siyo kubomoa mahusiano ya wanafunzi na walimu.
Sijui ni mwalimu gani ambaye ni mzazi anayeweza kumwadhibu mwanawe aliyekosa kushika kinyesi cha binadamu kama njia ya kumuonya.
Sisi tunadhani kwamba baadhi ya vurugu zinazojitokeza mashuleni husababishwa na walimu wenyewe kushindwa kufuata taratibu walizojiwekea wao wenyewe.
Tunakumbuka kwamba mwezi Februari mwaka huu, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Florina, wilayani Karatu, mkoani Manyara walivunja vioo vya madarasa na mabweni kufuatia madai yao dhidi ya uongozi wa shule hiyo kuwapa milo ya makande kila siku, kinyume na ratiba iliyopo.
Tunadhani kwamba wanafunzi wakiwa ni watu wazima, wasingeshindwa kukubali endapo uongozi wa shule ungewapa sababu zinazojitosheleza kuhusiana na kuwalisha makande kinyume cha utaratibu.
Kama hiyo haitoshi, mwezi Machi mwaka huu, itakumbukwa kwamba uongozi wa Shule ya Sekondari ya Lyamungo, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro uliwafukuza wanafunzi 50 waliobainika kushiriki katika mgomo na vurugu, hali iliyosababisha uharibifu mkubwa wa mali za shule.
Sisi tunashawishika kwamba baadhi ya vurugu kama hizi ambazo zinajitokeza mashuleni hazianzi kwa siku moja bali ni mfululizo wa malalamiko ya muda mrefu ambayo hupuuzwa na ngazi husika kuyapatia ufumbuzi.
Bodi za shule zina wajibu mkubwa kushirikiana na uongozi wa shule pamoja na ule wa wanafunzi ili kuweza kuzuia mahusiano mabovu kama hayo.
Bodi hizi ndizo zenye mamlaka ya kutoa maelekezo sahihi ya viwango vya adhabu ambavyo vinastahili kutolewa kwa wanafunzi badala ya kuwaachia walimu wenyewe ambao wengine huishia kujichukulia maamuzi kinyume na taratibu.
Inasemekana kuwa kuna baadhi ya shule, hususan za binafsi, hazina bodi kabisa.
Hili ni jambo hatari na linatakiwa wizara husika kufuatialia na kuhakikisha kwamba kila shule, hata kama ni ya chekechea inakuwa na bodi inayohusisha wazazi na wanafunzi pia kama wajumbe na kalenda ya vikao inafuatwa.
Kwa upande mwingine, wanafunzi nao wanatakiwa kuwa waadilifu na wanaozingatia sheria badala ya kufanya ghasia kama njia ya kupata ufumbuzi wa kero zao.
|