|
Uwajibikaji serikalini unazinduliwa usingizini kwa migomo?
2008-05-07 08:54:16
Na Grace Chilongola, PST
Kuna kila dalili kwamba, sasa kuna mfumo mpya wa utekelezaji ambapo imekuwa kama kawaida ya serikali kusubiri wananchi wake watoe vitisho kwa serikali yao kwamba wasipofanyiwa haya na yale watagoma.
Mwenendo huo wa maisha, umekuwa ukizaa matunda ambayo sasa kuna kila dalili kuwa waajiriwa wengi wa serikali wameutambua na labda kuuheshimu kuwa ni njia muafaka ya kufanya mawasiliano na mwajiri wao.
Yawezekana mtazamo huo ukawa sio sahihi kwa waajiriwa dhidi ya mwajiri wao, lakini kama haki haitendeki kwa mwajiriwa na kila akitumia njia za mazungumzo kwa muda mrefu hazizai matunda, kumbe afanye nini?
Na kama mwajiriwa anaona kuwa njia wanazotumia wengine zinaleta matunda yanayotakiwa katika kuleta unafuu fulani wa kupatikana kwa haki zao, kumbe wajifunze nini katika somo hilo jipya?
Kama mambo ndivyo yalivyo, kuna ulazima gani kwa serikali kusubiri vitisho toka kwa waajiriwa ili waweze kutoa haki zao wakati kuna baadhi ya waajiriwa wa serikali wenye dhamana fulani wamekuwa wakichota na kujilimbikizia mabilioni ya pesa bila kutazama wengine kama wanapata hata mlo mmoja kwa siku.
Serikali mara kwa mara imekua ikitoa ahadi mbalimbali kwa wananchi wake, lakini utekelezaji wake umekuwa wa kuvutana au ule unaofanywa kwa kasi ya kobe.
Hivi karibuni, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kushirikiana na wanachama wake walimu wa sekondari, vyuo na ukaguzi waliamua kuishinikiza serikali kuwalipa madai ya fedha zao mbalimbali zilizolimbikizwa ambazo imekuwa ikiwaahidi mara nyingi tena kimaandishi na kusainiwa na Waziri wenye dhamana na walimu.
Cha kushangaza ni kuwa, licha ya kusaini makubaliano hayo ya malipo na fedha kutengwa kwa ajili ya kufanyika malipo hayo bado wanaohusika wamekuwa wakisuasua katika utekelezaji wake na hivyo kuwasababishia wakati mgumu walimu.
Hata hivyo, baada ya kuona kuwa utekelezaji wake unakuwa mgumu, waliamua kutishia kuishinikiza serikali kwamba watagoma hadi madai yao yatekelezwe.
Msimamo huo ukaikurupusha serikali usingizini na kujipanga kwa kuchukua uamuzi wa haraka haraka kuanza kuwalipa madai hayo.
Na kweli baada ya siku si nyingi, baadhi ya walimu wakaanza kulipwa madai hayo huku wengine wakaahidiwa kuwa serikali inaendelea kuhakiki madai hayo ili utaratibu wa malipo ufanyike.
Pengine swali la kujiuliza, je iwapo fedha hizo zisingeanza kulipwa ina maana wahusika wangezibadilishia matumizi mengine na kuwaacha solemba walimu ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuelimisha taifa na kuwaachaa wakitaabika kwa kuzibiwa haki zao.
Hivi mwenendo huo wanaofanyiwa walimu ina maana mchango wao hautambuliwi vyema hata kufikia hatua ya kuwanyanyasa namna hiyo?.
Wanachokidai walimu ni haki yao na uhakiki ulikwishafanyika, je nini kiliingilia kati na kusababisha makubaliano ya kuanza kuwalipa yakapuuzwa na kuwa ndivyo sivyo?.
Kwa kuwa malipo ya walimu yamefanikiwa kutokana na tishio la mgomo ina maana sasa utaratibu mpya wa uwajibikaji serikalini ni kupitia migomo ndipo serikali istuke?.
Tukio la walimu kutishia kugoma na kufanikiwa ni moja ya matukio mbalimbali ya migomo ya kudai haki kwa baadhi ya watanzania katika sehemu zao za kazi ambayo sasa yanachukua mkondo mpya.
Hivi karibuni tena, watumishi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) chini ya mwekezaji mpya Rites ya India ambao wamekodishwa kuliendesha kwa miaka 25 walisimama kidete kutangaza mgomo na hata ikafikia hatua ya Waziri Mkuu,Mizengo Pinda kuingilia kati na malipo kufanyika haraka iwezekanavyo ndipo suluhu ikapatikana.
Hata hivyo, wakati anaingilia kati ni kwamba, tayari abiria wanaotegemea mno usafiri huo waliteseka sana na kujuta kwa kuadhibiwa kwa makosa ambayo siyo yao.
Hata hivyo, hakukuwa na namna nyingine baada ya majadiliano ya kutafuta suluhu yaliposhindikana zaidi ya njia hiyo ambayo ilizaa matunda.
Kimsingi huu uzalendo tunaouzungumzia kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu unakwamishwa na nani hasa hata kusababisha kuzuka kwa tabia mpya ya migomo?
Ifahamike kuwa walimu wananoa vipaji vya watu mbalimbali ambao baadaye watashika dhamana kubwa hata kuwa marais, wabunge na wengine ambao ni muhimu sana wanaowalea na kuwanoa watoto wetu walipwe kikamilifu na tena kwa wakati.
Hivi wabunge na mawaziri wasipolipwa malimbikizo kwa zaidi ya miaka mitatu katika hali ya kawaida kutakuwa na ufanisi katika utendaji wao au watashukaa morali na hata kuamua kufanya shughuli zao binafsi na kuacha ofisi wazi?
Je, kwa upande wa wabunge nao kama malipo yao yatacheleweshwa bila ya sababau za msingi kama ilivyo kwa walimu wanaotakiwa kwenda likizo na madai mwengineyo je watakuwa na amani moyoni?.
Vyombo vya habari hivi karibuni, viliandika na kutangaza habari za hatua zitakazochukuliwa na walimu iwapo siku ya Ijumaa Machi 18, hawatalipwa malipo yao na kusisitiza kwamba hakuna mabadiliko ya mgomo wa walimu utakaoanza Mei Mosi, mwaka huu na baadaye kutumia busara ya kuusitisha.
Kaimu katibu mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania, CWT, Bw. Ezekiel Olouch alisema kwenye mkutano wa walimu uliofanyika Tambaza sekondari kuwa, iwapo serikali isingewalipa fedha za walimu wa sekondari zinazofikia sh bilioni moja wangechukua hatua ya kwenda kuonana na Waziri mwenye dhamana ambaye ni Profesa Jumanne Maghembe.
Alisema serikali iliahidi kulipa madeni ya walimu katika siku 14 za mwezi Machi, mwaka huu baada ya CWT kukutana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Manejimenti, Utumishi wa Umma Bi. Hawa Ghasia.
``Tumekuwa tukipokea majibu ya kukatisha tamaa kutoka kwa Naibu Waziri wa Elimu na Waziri mwenyewe amekuwa akituchenga,`` alisema Bw. Olouch.
``Walimu walidhani kauli ya Profesa Maghembe ingeheshimiwa ya kuwalipa walimu ndani ya siku 14 za mwezi Machi, kauli iliyotolewa kimaandishi na serikali,`` alisema Bw. Olouch.
Ushirikiano wa walimu katika kuweka misimamo yao dhidi ya serikali yao imewawezesha walimu hao kuanza kulipwa malimbikizo yao siku iliyofuata yaani Ijumaa ya tarehe 18, Aprili, mwaka huu.
Hali hiyo inadhihirisha kuna uzembe wa namna fulani katika baadhi ya watumishi wanaohusika na ulipaji wa hundi hizo au serikali imezoea kuwalipa watumishi wake baada ya migomo.
|