|
Klabu saba zathibitisha kushiriki ndondi
2008-05-08 09:44:40
By Faustine Feliciane
Klabu saba za ngumi za ridhaa nchini tayari zimethibitisha kushiriki katika mashindano ya klabu bingwa ya taifa ya ngumi za ridhaa yaliyopangwa kufanyika Dodoma, Mei 26.
Akizungumza na Nipashe, Afisa Utawala wa Shirikisho la ngumi za ridhaa nchini (BFT) Saidi Adola alisema timu hizo zilizothibitisha kushiriki katika mashindano hayo zimeliandikia BFT barua za kuthibitisha ushiriki wao katika mashindano hayo.
``Napenda kutangaza kuwa mpaka kufikia leo tayari timu saba zimethibitisha kushiriki katika mashindano haya ya klabu bingwa ya taifa ambayo tumepanga kuyafanya Mei 26 mkoani Dodoma``, alisema Adola.
Aidha, Adola alizitaja klabu hizo zilizothibitisha kushiriki katika mashindano hayo na ambazo zimetuma majina 11 ya mabondia wake pamoja na uzito wao kuwa ni pamoja na Ngome, Magereza pamoja na JKT zote za Dar es Salaam.
Alizitaja timu nyingine kuwa ni Balhabou ya mjini Morogoro pamoja na timu mbili kutoka kwa wenyeji wa mashindano hayo ambapo moja wapo ni Dodoma Boxing Club (DBC).
Pia, Adola alisema BFT imeweka terehe ya mwisho ya klabu zote kuthibitisha kushiriki katika mashindano hayo ambayo ni Mei 15 na amezitaka timu zote kuhakikisha zinatuma barua zao za kuthibitisha kabla ya tarehe hiyo ambayo haitabadilishwa.
Aidha, alisema timu zote zitakazoshiriki katika mashindano hayo zinatakiwa kujigharamia nauli ya kwenda na kurudi kwenye mashindano ambapo BFT itagharamia malazi na chakula kwa timu hizo.
Pia alisema ili kufanikisha mashindano hayo, shirikisho hilo linahitaji zaidi ya Sh. milioni 30 kwa ajili ya kugharamia mashindano hayo ambayo yatatumika kuchagua wachezaji wa timu ya taifa watakaoandaliwa kwa ajili ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa ikiwemo michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012.
|