|
Abdi Kassim hatihati kuikosa Uganda
2008-05-08 09:45:52
By Somoe Ng`itu
KIUNGO mahiri na tegemeo wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Abdi Kassim `Babi` huenda akashindwa kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Uganda, The Cranes ambayo imepangwa kufanyika Mei 17 kwenye uwanja wa Namboole kutokana na kuwa na maumivu makali ya nyama kwenye paja.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa timu hiyo, Leopald Tasso Mukebezi alisema kuwa kutokana na maumivu hayo Abdi jana alipelekwa katika hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa picha (x-ray) ili kujua ukubwa wa tatizo na kuweza kupatiwa matibabu.
Tasso alisema kuwa kutokana na hali hiyo mchezaji huyo ameshindwa kuendelea na mazoezi mpaka pale atakapopona.
``Katika kikosi chetu (Stars) kuna majeruhi watatu, Uhuru Selemani, Henry Joseph na Babi, lakini Babi leo (jana) ilibidi apelekwe hospitali ili kufanyiwa uchunguzi zaidi,`` alisema meneja huyo.
Aliongeza kuwa katika timu hiyo bado wachezaji watatu ambao hawajaripoti kambini ambao ni pamoja na Haruna Moshi `Boban`, Meshack Abel na Erasto Nyoni.
Nyota hao wanaocheza soka ya kulipwa Oman na Rwanda wameitwa kujiandaa pamoja kwa ajili ya mechi dhidi ya Mauritius ambayo itafanyika Mei 31 kwenye Uwanja Mpya wa Kisasa hapa jijini Dar es Salaam huku wengine wanaocheza ligi ya hapa nyumbani wakijinoa dhidi ya mechi ya The Cranes.
Katika mechi ya kwanza iliyofanyika jijini Mwanza, Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na hivyo inahitaji sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele kwenye mashindano hayo.
Mshindi katika mchezo huo atakutana na mshindi kati ya Rwanda na Sudan.
|