|
Ruvuma, Lweru Eagles zapita
2008-05-08 09:47:00
By Jimmy Charles
Timu ya soka ya mkoa wa Ruvuma, Ruvuma Warriors jana iliitoa kwa taabu timu ya Kigoma Stars
katika mchezo wa mtoano wa Kombe la Safari Lager Taifa Cup uliochezwa uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.
Ruvuma ilianza mchezo huo kwa kasi na kujipatia bao lake katika dakika ya pili lililofungwa na Iddi Ajilo baada ya kupokea pasi ya Ally Jaza.
Jaza baadae aliongeza bao la pili katika dakika ya 29 baada ya kuwatoka mabeki wa Kigoma na kipa Omar Sebabiu.
Kigoma iliweza kupata bao lake dakika moja baadae lililofungwa kwa penati na Hussein Soud katika dakika ya 30 iliyotolewa na mwamuzi Aden Mbaga wa Dar es Salaam baada ya Omar Mussa wa Kigoma kuchezewa vibaya na Abdalla Ausi.
Bana Prosper aliweza kusawazishia Kigoma iliyoingia kipindi cha pili kwa nguvu baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Issa Seba katika dakika ya 71.
Kigoma, baada ya bao hilo ilicharuka zaidi lakini ikajikuta inapachikwa bao kwa penati katika dakika ya 88 iliyofungwa na Ausi Abedi.
Hata hivyo, Kigoma ilipata bao katika dakika za majeruhi, ambalo lilikataliwa na mwamuzi msaidizi John Kanyenye wa Mbeya kwa madai mfungaji Seba alikuwa ameotea, kitendo kilichowakasirisha wachezaji wa Kigoma na mashabiki wachache waliofika kushuhudia mchezo huo.
Mohamed Kapombo wa Kigoma ndio aliibuka mchezaji bora katika mchezo huo kutokana na kujipatia kitita cha sh. 50,000.
Wakati huo huo, timu ya mkoa wa Kagera, Lweru Eagles jana ilifanikiwa kuitoa timu ya mkoa wa Tanga, Mkwakwani Stars kwa kuichapa 1-0.
Bao la Lweru Eagles lilijazwa kimiani na Paul Kabonga katika dakika ya 75 baada ya kupokea pasi ya Juma Seif, ambaye aliondoka na kitita cha sh. 50,000 kutokana na kuibuka mchezaji bora.
Leo timu ya Tabora `Mashujaa wa Unyanyembe` inavaana na Mwanza itakayoanza saa nane mchana na katika mchezo wa pili, Lindi itakwaana na Ilala.
|