08 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Huu ni muda wa kuwawajibisha viongozi washirikina kama hawa
 
2008-05-08 10:13:35
Na Mhariri

TABIA ya baadhi ya watu wanaojifanya ni waganga wa kienyeji wenye uwezo wa kuwabaini wachawi inaonekana kukomaa katika baadhi ya maeneo nchini, ambapo kama hatua madhubuti hazitachukuliwa mapema, inaweza kuzua madhara makubwa kwa wananchi.

Kwenye toleo letu la jana tuliandika habari kwamba katika hali isiyokuwa ya kawaida, wananchi wa Kitongoji cha Igunguli, Kata ya Fufu, Wilaya ya Chamwino, walichangishwa kwa nguvu kila mmoja Sh. 1,500, ili kugangwa dhidi ya wachawi.

Taarifa kutoka kitongoji hicho zilisema kuwa mganga `anayewagangua` alitafutwa na viongozi wa kitongoji hicho, kwa ajili ya kuwaondolea nuksi na kusafisha wachawi, ambapo amedaiwa kutumia wembe mmoja kuchanja msululu wa wananchi kichwani na kwenye makalio.

Baadhi ya wananchi wa kitongoji hicho walikaririwa wakisema kuwa viongozi wao, Bw. Yahaya Njalamoto ambaye ni Mwenyekiti na Katibu wake, Ngage Msangi wakishirikiana na Diwani wa Kata hiyo, Bw. Meshaki Songo, waliitisha mkutano wa kijiji na kuwataka wananchi watoe michango hiyo.
Imedaiwa kwamba hatua hiyo ilikuja kufuatia malalamiko kuwa vitendo vya ushirikina vimekithiri katika kijiji hicho na kusababisha biashara zao za samaki kuathirika.
Imeelezwa kwamba, baada ya mkutano huo, wananchi walichanga jumla ya Sh. 470,000 na kumpatia mganga huyo ambaye alianza kazi ya kuwapatia chanjo wananchi hao, ili kuwaondolea mikosi na kuwakinga na vitendo vya ushirikina.
Baadhi ya wananchi waliokataa kushiriki katika tukio hilo, walisema kwamba wamekuwa wakitishiwa maisha na mganga huyo na viongozi wa kitongoji hicho wakidaiwa kuwa wao ndio wachawi.
Mganga huyo aliyefahamika kwa jina moja la Shaibu, anayedaiwa kutokea katika kijiji cha Lifua, Wilaya ya Ludewa, alikuwa akifanya shughuli zake hizo za \'kugangua\' uchawi kwenye Ofisi ya Chama cha Mapinduzi ya kitongoji hicho.
Labda huu unaweza kuwa ni mfano mmoja tu kati ya matukio mengi kama haya nchini ambapo hata viongozi wa umma hushirikiana na waganga wa aina hiyo kwa ajili ya kuwafanyia utapeli wa waziwazi wananchi.
Mara nyingi, mbali na wananchi kutapeliwa pesa zao, ukamataji wa wachawi umekuwa ukisababisha kuvunjika kwa amani kwa wale wanaotuhumiwa.
Tumeandika mara kadhaa habari za wanakajijiji kuchomewa nyumba zao na mali zao kutokana na tuhuma kama hizi zisizo za kisayansi. Katika maeneo mengi yametokea hata maafa.
Katika Kitongoji cha Igunguli, baadhi ya wananchi wakiwemo viongozi wao, eti wanahisi wanarogwa na kwamba ndio chanzo cha biashara yao ya samaki kutoenda vyema.
Inashangaza sana kuona viongozi wa kijiji akiwemo diwani, wakitumia njia kama hii ya mkato ambayo kimsingi ni ya kitapeli, badala ya kutafuta sababu za kisayansi zinazosababisha kupungua kwa mapato.
Katika tukio hili, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na madai ya wembe mmoja kutumika kuchanjia msululu wa wananchi. Mungu apishilie mbali, lakini kitendo hicho kinashangaza sana kwani kinaweza kuwa sababu ya wananchi hawa kuambukizana magonjwa hatari, ukiwemo Ukimwi.
Kitendo cha viongozi wa kitongoji hicho kuhamasisha michango isiyokuwa halali kwa ajili ya utafutaji wachawi kwa hakika kimekwenda kinyume cha taratibu na sheria za nchi kwa kuchochea uvunjwaji wa amani.
Sisi tunajiuliza, wao kama viongozi walipata kibali wapi kiasi cha kuwalazimisha wananchi kuchangia shughuli zisizokuwa halali na zinazohatarisha maisha yao?
Ni matarajio ya walio wengi kwamba uongozi kuanzia ngazi ya wilaya ya Chamwino unastahili kuangalia uzito wa kashfa hiyo na kuwajibika ipasavyo kutokana na kuruhusu uongozi wake wa chini kushabikia ushirikina.
Zaidi ya hayo, tunadhani viongozi na waganga walioshiriki kwenye zoezi hilo wana tuhuma za kujibu, ikizingatiwa kwamba vifaa vilivyotumika kuwachanja siyo salama kiafya na michango iliyokusanywa ni kinyume cha sheria.
Wananchi nao, hususan wale wasiokubaliana na ujinga kama huu, wanatakiwa kutoa taarifa za waganga wa aina hiyo kwenye vituo vya polisi mara wanapowabaini ili kuwezesha kukamatwa kwao na kufikishwa mbele ya sheria.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.