|
Ukataji miti umeua maeneo chepe Pwani
2008-05-08 10:15:42
Na Amri Lugungulo
Ukosefu wa elimu ya utunzaji wa mazingira umesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na ukataji miti kwa ajili ya kuanzisha mashamba na kwa ajili ya matumizi mengine hasa uchomaji wa mkaa hadi kuleta tishio la mkoa wa Pwani kukabiliwa na jangwa.
Hata hivyo elimu ya utunzaji wa mazingira imewafanya wakazi wake hivi sasa kuwa na mwamko wa kuotesha miti na kuhifadhi mazingira ambapo mwaka huu mkoa umepanga kuotesha miti milioni kumi. Mwandishi Amri Lugungulo wa Shirika la Habari la PST anaelezea zaidi katika makala haya.
Elimu ya utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa kila mkazi wa mkoa wa Pwani kutokana na kubainika kuwa kasi ya kuharibika kwa mazingira imesababishwa na ukosefu wa elimu hiyo kwa vizazi mbalimbali vikiwemo vya sasa na vya zamani.
Miaka ya nyuma, mazingira yalikuwa yakiharibiwa na wazee kutokana na kilimo cha kukata miti ovyo, bila ya kutambua kuwa walikuwa wakifanya uharibifu wa mazingira na hatimaye kukosekana kwa mvua za kutosha.
Kizazi cha sasa, mbali ya kuendelea na kilimo hicho cha kukata miti hovyo, pia wameongeza kasi ya kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, kupasua mbao,magogo, kuni, fito na nguzo hatimaye mazingira mkoani yanazidi kuharibika.
Hivi karibuni wakazi wa kijiji cha Chole wilayani Kisarawe, mkoani humo wakiongozwa na Kaimu Mkuu wa mkoa huo, Bw Gilbert Msagama Dololo, waliadhimisha kimkoa siku ya upandaji miti kitaifa.
Bw. Dololo akimwakilisha mkuu wa mkoa huo, Dk. Christine Ishengoma, aliwaongoza wanakijiji wa Chole kupanda zaidi ya miche 900 ya miti aina ya mninga na mkuyu katika bonde la Kirobo lililopo kati ya kijiji cha Kwala na Chole wilayani Kisarawe.
Katika shughuli hiyo alikuweko mzee Waziri Mbegu Kirobo, mwenye umri wa zaidi ya miaka 80 ambaye ni mtoto wa mzee Mbegu Kirobo aliyeweka makazi yake katika eneo hilo miaka ya nyuma hatimaye eneo hilo likaitwa kwa jina lake.
Hivi sasa, Bw. Waziri Mbegu Kirobo, ambaye anamiliki eneo hilo lililo karibu na bonde hilo la Kirobo, aliimbia PST kuwa mazingira ya bonde hilo yaliharibiwa na wazee enzi hizo za zamani kutokana na kilimo cha kukata miti.
Awali bonde hilo lilikuwa na msitu mkubwa na maji yalikuwa yakipatikana kwa urahisi kwenye visima vifupi, lakini baadaye visima vilikauka kutokana na miti mingikukatwa na kuliacha eneo hilo likiwa tupu.
Kwa sasa uongozi unapanda miche ya miti ili kurudisha mazingira kama yalivyokuwa zamani.
Alisema wazee wa zamani, bila ya kutambua nini walichokuwa wakifanya kutokana na kukosa elimu ya utunzaji wa mazingira na umuhimu wake walifyeka bonde hilo kama walivyokuwa wakifanya wazee wa maeneo mengine mkoani humo na kusababisha kugeuka kuwa nusu jangwa hali iliyochangia kuongezeka kwa ukame.
Kutokana na ukosefu wa elimu ya utunzaji wa mazingira, kila mwaka baadhi ya wazee walikuwa wakianzisha kilimo hicho cha kufyeka misitu ambapo mashamba yake yalikuwa yakiitwa \"chenge\" na hivyo kuendelea kusababisha uharibifu wa mazingira na ukame kubisha hodi.
\"Enzi hizo nilipokuwa mtoto, bonde hili linaloendelea katika vijiji hivi vitatu vya Kwala, Chole na Panga la Mwingireza, palikuwa na uoevu mzuri na uoto wa miti.\"
Bw. Kirobo anasema wakati mwingine walikuwa wakikatazwa kwenda eneo hilo kwa kuhofia kuwa wangeweza kuzama kwenye ardhi chepe chepe.
\"Lakini ghafla hali hiyo ilitoweka na sasa tunakabiliwa na uhaba wa maji kwenye visima. Watu wanakesha
visimani kusubiri maji\", anasema.
Hata hivyo hivi sasa yuko mstari wa mbele wa kutunza mazingira baada ya kupata elimu hiyo na kutambua umuhimu huo.
\'Elimu hii ninayoipata kutoka kwa wajukuu zangu ambao ni ninyi, naitilia maanani na kwamba ni muhimu elimu hii ikaendelezwa kila mtu mkoani mwetu ili kujinusuru na balaa la ukame kutokana na ukosefu wa mvua za kutosha mkoani mwetu,\"anasema Mzee Kirobo.
Mzee Kirobo anashauri baadhi ya wajukuu zake ambao wengi ni vijana kuacha kuhariu mazingira kwa kukata miti ovyo ili kuepukana na balaa hilo ambalo wakati linaweza likaleta balaa lingine la njaa na maradhi licha ya ukame.
Anasema wazazi wake kama wangekuwa na elimu hiyo ya kutunza mazingira kamwe pasingekuwepo na uharibifu wa mazingira na badala yake maeneo mengi kungekuwa na misitu na kwa vyovyote ukame usingekuwepo.
Katika maadhimisho hayo, Mkuu wa mkoa huo, Dk. Ishengoma aliwapongeza wakazi wa mkoa huo kwa kupanda zaidi ya miti milioni 16 tangu kampeni ya kitaifa ya upandaji miti ilipozinduliwa Aprili, mwaka 1999 na mwaka huu zaidi ya miche ya milioni kumi pia inatarajwa kupandwa mkoani kote.
Hata hivyo Dk Ishengoma alionya uvunaji holela wa miti kwana anasema ni kikwazo cha maendeleo, hivyo kuwataka viongozi mkoani kudhibiti hali hiyo hususani ya ukataji miti kwa
ajili ya mkaa.
\"Viongozi na wananchi vijijini mkilifahamu hili, kuwa si muda mrefu litatokea, hamtaruhusu uvunaji holela unaoendelea kwa wakati huu kwani hamtakuwa na mahali pa kuishi, kuhamia wala kukimbilia nyinyi na familia zenu,\"alisema Dk Ishengoma.
Mapema Katibu Tawala Msaidizi na mshauri wa wa maliasili sekretarieti ya mkoa huo, Bw Johansen K.Bukwali amesema miche ya miti katika halmashauri za wilaya zote sita mkoani humo imepandwa na watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizokuwa za serikali.
Miti hiyo iliyopandwa kwa ajili ya kutaka kuvuna mbao, nguzo, kuni, matunda, mapambo, ujenzi na mazao ya biashara.
Mkoa wa Pwani una misitu 44 inayohifadhiwa katika wilaya zote sita za Kisarawe, Mkuranga, Rufiji, Mafia, Bagamoyo na
Kibaha ikiwa na eneo la hekta 335,712 kwenye ardhi huria lenye ukubwa wa hekta milioni 2.2 linategemewa na wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa mazo ya misitu kwa matumizi ya nishati, ujenzi, mbao na kuni.
Hata hivyo Bw Bukwali anasema ingawa ngawa viongozi wanajitahidi kueleza athari za uharibifu wa mazingira kutokana na uvunaji ovyo wa mazao ya misitu, jamii mkaoni humo
kuziba masikio na kuendelea kukaribisha athari hizo za ukame kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa mazao hayo ya misitu.
Akiungana na Mzee Kirobo wa kijiji cha Chole juu ya umuhimu wa kutunza mazingira, Bw Bukwali anasema kuwa endapo wanyeviti na watendaji wa ngazi mbalimbali wa vijiji watazingatia elimu ya utunzaji mazingira na kusimamia utekelezaji wa masharti ya kuweza kudhibiti uvunaji holela wa mazao hayo janga la ukame litapungua mkoani Pwani.
|