|
Nsajigwa kutoichezea Stars
2008-05-09 08:50:41
By Somoe Ng\'itu
Beki wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa hatacheza katika mchezo wa kwanza wakati Stars itaumana na Mauritius katika mchezo wa Kundi A wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2010 kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Nsajigwa alipata kadi hiyo mwaka jana wakati Stars inacheza na Burkina Faso ikisaka nafasi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika zilizofanyika Ghana mwaka huu, ambapo ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo huo, ukiwa ni ushindi pekee kwa timu hiyo ugenini.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Stars, Marcio Maximo alisema kuwa Nsajigwa atakuwa nje katika mchezo huo uliopangwa kufanyika Mei 31 kwenye uwanja wa kisasa baada ya kupokea taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Afrika, CAF.
Maximo alisema kuwa CAF imeeleza kuwa beki huyo alianza kuitumikia adhabu hiyo katika mechi dhidi ya Msumbiji mwaka jana na hii ya Mauritius ndio atakuwa anamalizia adhabu hiyo.
Hatahivyo kocha huyo alisema kuwa anaweza kumpanga Nsajigwa katika mechi ya marudiano dhidi ya Uganda, The Cranes, Mei 17 endapo atakuwa amerejea katika kiwango chake cha kawaida.
``Unajua mashindano haya yamefuatana, kwa hiyo Shadrack anaendelea kufanya mazoezi kwa nguvu na wenzake na akiwa katika nafasi nzuri naweza kumpanga katika mechi ya Uganda,`` alisema Maximo.
Aliongeza kuwa hamasa iliyopo katika kikosi chake ni ya hali ya juu ambapo inamfanya awe na matumaini ya kushinda katika mchezo huo na kuiondoa Uganda.
Wakati huo huo, Maximo alisema kuwa hataweza kuhudhuria katika mechi za mashindano ya Kombe la Taifa yanayoendelea kwenye uwanja wa Taifa kutokana na kukumbwa na programu ya mazoezi ya Stars.
Maximo alisema kuwa mashindano hayo ni nafasi pekee kwa makocha na viongozi wa klabu kuyatumia kupata wachezaji watakaowasajili na yeye kuja kuwaona katika mechi za klabu na huo ndio utaratibu unaoheshimiwa na makocha wengi duniani.
|