|
Ilala yaiingiza mjini Lindi
2008-05-09 08:51:13
By Jimmy Charles
Timu ya Ilala jana ilitoa onyo katika mashindano ya taifa yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kuiingiza mjini Lindi kwa kuifunga 10-1, katika mchezo wa mashindano hayo.
Kwa ushindi huo, mkoa wa Ilala sasa utacheza na Mwanza ambayo katika mchezo wa awali jana iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tabora katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja huo huo.
Mabao ya Ilala inayoundwa na wachezaji wengi wa Simba yalifungwa na Mussa Hassan Mgosi aliyetingisha nyavu mara tano katika dakika ya 21, 34, 35, 37 na 47 na kujipatia mpira baada ya mchezo huo.
Mabao mengine ya washindi yalifungwa na Credo Mwaipopo katika dakika ya kwanza huku mchezaji huyo akiibuka na sh. 50,000 baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo ambao pia ulishuhudiwa na watazamaji wachache sana.
Ramadhani Chombo naye aliifungia Ilala katika dakika ya 12 kabla ya Athumani Machupa kufunga bao la saba katika dakika ya 35 na lile la 10 likijazwa wavuni na Mohamed Kijuso katika dakika ya 87.
Lindi ambayo imeyaaga mashindano hayo, iliandika bao lake la kufutia machozi katika dakika ya baada ya mabeki wa Ilala na kipa wao Juma Kaseja kufanya uzembe kuokoa mpira huo.
Mashindano hayo ambayo bingwa wake ataondoka na kitita cha sh. milioni 30 yataendelea tena leo kwa timu ya mkoa wa Pwani kumenyana na Kilimanjaro katika mchezo wa awali kabla ya Morogoro haijapepetana na Dodoma.
|