|
Kondic azua balaa Yanga
2008-05-09 08:52:23
By Mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga Dusan Kondic, ametoa mtihani mgumu kwa viongozi wa klabu hiyo baada ya kuweka wazi kuwa ni lazima ampate mchezaji wa Simba Kelvin Yondani pamoja na Stephen Mwasika wa Prisons ya Mbeya.
Kondic, ametoa mtihani huo baada ya kuwasilisha mapendekezo yake ya usajili katika kuimarisha kikosi chake kinachotarajia kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Huo umekuwa ni mtihani kutokana na viongozi wa klabu ya Simba kuweka wazi kuwa hawako tayari kumuachia mchezaji huyo, ambapo walisema wameshaingia nae mkataba kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
Kwa mujibu wa habari za ndani toka kwa mmoja wa kiongozi wa klabu hiyo aliyekataa jina lake kuandikwa gazetini alisema kuwa mapendekezo yaliyowasilishwa na Kondic ni mtihani mkubwa ambao unaweza kuzirudisha Yanga na Simba kwenye sakata kama la Athuman Idd.
``Kocha ameshawasilisha mapendekezo yake ni mazuri na yenye manufaa kwa timu lakini sasa ukijakuangalia kwenye suala zima la kuwaopata hao wachezaji hasa Yondani hali inakuwa tofauti, tunaweza kumlipa lakini je klabu yake ya sasa itakubali,`` alihoji kiongozi huyo.
Alisema kuwa pamoja na suala hilo kuwa gumu tayari uongozi unafikiria kukaa na Kamati ya Usajili ili kuliangalia kwa kina suala hilo pamoja na kufuatilia wachezaji wengine waliotakiwa na Kocha.
Alisema kwa upande wa Mwasika hilo linawezekana kutokana na kubaini kuwa mchezaji huyo si muajiriwa wa Jeshi la Magereza, ambapo alikuwa akiitumikia timu hiyo kama raia.
Aidha, alisema kuwa Kondic pia amependekeza kupatiwa wachezaji wa kimataifa zaidi ya wawili, ambao watasaidia kukiimarisha kikosi cha timu hiyo.
Mwenyekiti wa Klabu hiyo Imani Madega, hivi karibuni alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa Yanga kwa sasa inaouwezo wa kumsajili mchezaji yeyote bila kujali gharama.
Hata hivyo, aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mserbia Micho aliwaasa Yanga kusajili wachezaji wenye viwango, lakini sio wale wanaotoka nchi jirani ya Kenya kwa kuwa ni wasumbufu wakubwa.
|