|
Mikakati ibuniwe kufufua riadha
2008-05-09 08:54:34
Na Mhariri
Tanzania iliambulia patupu kwenye michuano ya riadha ya Afrika iliyomalizika hivi karibuni nchini Ethiopia.
Nchi yetu imeboronga wakati mashindano hayo yalikuwa ndio sehemu ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika baadae mwaka huu .
Kibaya zaidi, mwakilishi wa Tanzania alichelewa kufika hata kwenye mashindano yenyewe licha ya kulipiwa nauli na malazi na waandaaji wa mashindano hayo.
Ni fedheha kubwa kutokana na ukweli kwamba wadau wa riadha ulimwenguni miaka yote wameichukulia kuwa Tanzania ina vipaji vya riadha lakini haviendelezwi.
Matarajio hayo yanatokana na ukweli kuwa katika miaka ya 1970 na 1980 ulikuwa hauwezi kuacha kuitaja Tanzania katika mashindano makubwa ya riadha.
Tunakumbuka historia ya huko nyuma, ambapo kwa mfano Filbert Bayi, ambaye ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki nchini (TOC) alikuwa tishio.
Mwaka 1973 alivunja rekodi ya Afrika ya Mkenya Ben Jipcho katika mbio za mita 1500 wakati Michezo ya Afrika iliyofanyika nchini Algeria.
Mwaka uliofuata alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 iliyokuwa inashikiliwa na John Walker wa New Zealand wakati wa michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Christchurch, New Zealand.
Walikuwepo wakati huo wanadai kuwa Bayi alifanya maajabu kutokana na kuanza mbio hizo kwa kasi bila ya kuchoka na hadi kuweza kuvunja rekodi hiyo ya dunia.
Kitu zaidi ni kuwa rekodi ya Bayi ilidumu kwa miaka mitano hadi pale Sebastian Coe alipovunja rekodi hiyo mwaka 1979 mjini Roma, Italia.
Bayi baadae aliweza kupata medali ya fedha ya Olimpiki katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi katika michezo iliyofanyika mwaka 1980 huko Moscow.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la riadha nchini (RT), Suleiman Nyambui alikuwa kinara katika mbio za mita 5,000 na na kupata medali ya fedha katika michezo ya Olimpiki mjini Moscow.
Nyambui pia alikuwa aking\'ara duniani katika mbio za ndani za mita 5,000.
Bado tuna akina Gidamis Shahanga, Zacharie Barie, Juma Ikangaa, Nzael Kyomo, Amosi Malundi, Morris Okinda, Mwinga Mwanjala, Claver Kamanya, Mossi Ally na wengi wengineo waliong`ara mno kimataifa.
Toka enzi ya nyota hao, nchi yetu imeonekana kupoteza mwelekeo katika mchezo huo.
Inasikitisha kuwa nchi yetu imesheheni mikoa, ambayo ingeweza kutoa wanariadha nyota duniani, lakini wanashindwa kuendelezwa na kutiwa moyo.
Kwa mfano mikoa ya Mara na Kagera huko nyuma ilikuwa na sifa ya kutoa warusha mikuki wazuri.
Mikoa ya Arusha, Dodoma na Singida wana sifa ya kutoa wanariadha wa mbio ndefu wakati mikoa ya Iringa na Mbeya ina wanariadha wazuri wa mbio za kati.
Mkoa wa Mwanza una sifa ya kutoa wanariadha wakali wa mbio fupi.
Tatizo la Tanzania limekuwa ni mipango duni, ambapo wanamichezo wake wanaandaliwa kwa kukurupuka zaidi.
Hata Rais wa Shirikisho la riadha la Afrika (CAA), Hamad Kalkaba Malboum ameahidi shirikisho linaangalia uwezekano wa kuisaidia Tanzania kufufua riadha.
Hata hivyo, alisema tatizo la viongozi wa RT hawajawa wazi na mipango yao ya kuuendeleza mchezo huo.
Ndiyo maana tunaona kwamba kuna haja ya makusudi sasa kwa RT kujikita katika kuangalia mipango ya muda mrefu ili Tanzania iweze walau kujitoa kimasomaso kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012 itakayofanyika London, huku pia kukiwa na matumaini ya kupata medali katika michezo ya Olimpiki huko Beijing, China, baadaye mwaka huu.
|