09 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Uchumi hautakuwa ipasavyo kama ujenzi wa barabara unasuasua
 
2008-05-09 08:56:55
Na Simon Mhina

Katika kitabu chake - The End of Poverty, Profesa Jeffrey D. Sachs anaeleza kuwa mikakati yote ya kupambana na umaskini haitaweza kuzaa matunda ikiwa maendeleo ya barabara yatapewa kisogo.

Prof. Sachs ambaye anasifika duniani kwa kusaidia mipango na mikakati ya kupambana na umasikini duniani, akiwa amesaidia nchi nyingi kujikwamua kiuchumi, anasema Tanzania inao welekeo mzuri wa kupunguza umasikini zaidi ya nchi nyingi za Afrika, lakini inakosa barabara nzuri.

Akiwa ametembelea pia Tanzania, Prof Sachs anasema barabara nyingi za Tanzania, zikiwemo hata za mijini, ziko katika hali mbaya hivyo kuwa kikwazo kusaidia msukumo wa kupunguza umasikini.

Anasema ikiwa msukumo wa kuwa na barabara bora- za mijini na vijijini, Tanzania ingeweza kabisa kuwa mfano bora wa kutokomeza umasikini na kufikia, kwa kiasi kikubwa Malengo ya Milenia.

``Kuna kila sababu ya Tanzania kuwa na watu wenye maisha bora zaidi kuliko nchi nyingi masikini, kinachotakiwa kuhimizwa ni barabara bora- kwani madini yapo, watu wanajituma zaidi mashambani, lakini wanakosa namna ya kuuza mazao yao, namna ya kufika maeneo ya huduma mbalimbali kwa wakati,`` anasema mwanazuoni huyo Mwingereza.

Mtazamo huo umetafsiriwa vyema katika Mpango wa Kupambana na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA), ambao malengo yake yanatakiwa yawe yametimia ifikapo mwaka 2010.

MKUKUTA umejikita zaidi vijijini, ambako asilimia 80 ya Watanzania ndiko wanakoishi.

Kwa hilo MKUKUTA unalega kwamba ifikapo 2010 Tanzania iwe imejiwekea uwezo wa kukarabati kilometa elfu kumi na tano (15,000km) kila mwaka, badala ya kilometa 4,500 zinazokarabatiwa sasa.

MUKUKUTA pia unahitaji ifikapo mwaka 2010, asilima 75 ya barabara za vijijini ziwe zinapitika badala ya asilima 50 ya sasa. Aidha mpango huo unasisitiza kupunguzwa kwa ukosefu wa ajira, kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000, kufikia asilimia 6.9 ifikapo mwaka 2010.

Raisi Kikwete amekuwa akiahidi kukamilishwa kwa miradi ya barabara iliyoanzishwa kabla ya serikali yake kuingia madarakani na kuwa serikali yake imeanzisha miradi mipya ya barabara, hata hivyo maendeleo ya barabara nyingi za vijijini yamekuwa na kasi ndogo kutokana na ufinyu wa bajeti.

Serikali mara zote inaeleza kuwa ufinyu wa bajeti unakwamisha mipango mingi ya maendeleo ya barabara, hivyo kuwa kikwazo cha kufanikiwa kwa mikakati ya maendeleo, na ile ya MKUKUTA inayokusudiwa.

Wabunge kwa upande wao, wamekuwa wakieleza kusikitishwa kwao na ubovu wa barabara katika maeneo wanayoyasimamia na kwamba hali hiyo, pamoja na kuizungumza bungeni, bado haisaidii sana kwa kuwa ufinyu wa bajeti unakwamishwa.

``Pamoja na kuwepo kwa barabara nzuri, moja au mbili hasa maeneo ya kati ya makao makuu ya wilaya na njia kuu zinazounganisha mikoa, bado barabara nyingi za vijijini ni mbaya. Hali hiyo inakwamisha sana maendeleo ya wananchi na kufanya uwepo wa ugumu wa kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanafikiwa haraka iwezekanavyo,`` anasema Mbunge wa Busega, Dk Raphael Chegeni.

Madiwani nao wamekuwa wakililia ufinyu wa bajeti ili kutengeneza barabara za maeneo yao.

Madiwani wanaolalamika sio wa vijijini peke yao ni pamoja na wale walioko katika majiji au mijini kama vile Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Tanga na maeneo mengine yenye wakazi wengi na kuwepo kwa shughuli nyingi za kukuza uchumi kama vile viwanda na nyinginezo.

Umefika wakati tujiulize; ni kwa nini kila bajeti ya ujenzi na ukarabati wa barabara inapoongezeka lakini ni vigumu kuhisi mabadiliko?

Wakati umefika kwa serikali na wadau wengine wa barabara nchini kufikiria na kujaribu matumizi ya teknolojia mbadala ya kisasa ya kutengeneza barabara imara, rahisi na inayochukua muda mfupi kukamilisha ujenzi au ukarabati.

Barabara hizo zinazotumia teknolojia ya kisasa hazihitaji bajeti kubwa, kama ilivyo kwa barabara za lami ambazo hugharimu kiasi kikubwa cha fedha, muda mrefu, vifaa vingi vya kutenda kazi pamoja na idadi kubwa ya wafanyakazi, na wenye ujuzi wa hali ya juu.

Katika utaalamu huo wa ujenzi wa barabara za kisasa, hakuna lami inayohitajika, isipokuwa ni kukusanywa kwa mchanga ulioko katika barabara husika au mwingine wowote na baadaye kumiminwa kwa dawa maalum ambayo hufanya mchanga au udongo wa barabara kushikana zaidi na kuifanya kuwa imara.

Dawa inayotumika hapa ni Romix Soilfix na surface seal ambazo zimetengenezwa kitaalamu kushikamanisha udongo na kuufanya kuwa imara zaidi, huku barabara zilizotengenezwa kwa utaalamu huo zikidumu kwa muda mrefu.

Mara baada ya barabara kuwekwa Romix Soilfix na surface seal kinachofuata ni kuwekwa kwa BTA - ambayo ni mchanganyiko mwingine wa dawa unaofanya barabara kuwa na weusi huku ikionekana kama imewekwa lami.

BTA si lazima iwekwe wakati huo huo bali barabara inaweza kuendelea kutumika bila BTA, na uwezo wa kifedha ukiruhusu, BTA inawekwa baadaye.

Uimara wa barabara zilizotengenezwa kwa utaalamu huu, umethibitika na kukubalika kwa nchi nyingi za Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Sudan, Nigeria, Zambia, Angola na Msumbiji.

Katika nchi hizo, barabara hizo zimetambulika kuwa ni mkombozi wa fedha nyingi za serikali ambazo awali zilikuwa zikitumika kukamilisha barabara aghali za lami.

Nigeria hadi sasa ndiyo inayoongoza Afrika kwa ujenzi wa barabara za kisasa zinazotumia Romix, ikiwa na zaidi ya kilomita 1,000 za barabara hizo.

Akiwa bado madarakani, Rais Olusegun Obasanjo aliwahi kukaririwa akieleza kuwa, kugundulika kwa barabara hizo na kuanza ujenzi wake, Nigeria imeokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zilikuwa zikitengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami.

Mbali na nchi hizo, Marekani imekuwa ikitumia utalaamu huo wa ujenzi wa barabara nchini Irak, katika mpango wake maalum wa kuinua uchumi wa Irak baada ya kumuondoa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Saddam Hussein.

Inaaminika kuwa kujenga kilomita moja ya barabara ya lami huigharimu serikali, kupitia Wakala wa Barabara (Tanroads), Serikali Kuu zaidi ya sh bilioni moja, muda mrefu kukamilika kwa mradi na zaidi sana kutumika kwa vifaa vingi na aghali kukamilisha kazi hiyo.

Endapo utatumika utaalamu wa kisasa wa ujenzi wa barabara imara kwa kutumia bidhaa na tekinolojia ya Romix, serikali inaweza kuokoa zaidi ya asilimia sitini ya gharama, kwani gharama za ujenzi wa barabara za kisasa ni kubwa mno.

Gharama zinazoweza kuokolewa, ikiwa serikali au kupitia kwa wakala itaamua kutumia utaalamu wa ujenzi wa barabara za kisasa, zinaweza kuelekezwa katika maeneo mengine ya maendeleo ikiwamo kuimarisha elimu, kuboresha huduma za afya na zaidi sana kuihakikishia Hazina ya Serikali uwepo wa fedha za kutosha kwa shughuli za kupunguza umasikini.

Kikubwa zaidi katika matumizi ya teknolojia za namna hii ni ushirikishwaji wa wananchi katika ujenzi au ukarabati wa barabara.

Katika Tanzania, barabara za mfano za utaalamu huo zimejengwa Zanzibar- Unguja na Pemba ambapo imethibitika namna kiasi kikubwa cha fedha kinaweza kuokolewa kwa kuanzisha miradi ya ujenzi wa barabara za namna hiyo.

Injinia wa Matengenezo ya Barabara, Zanzibar, Japhet Malambi (UUB) anasema utaalamu huo wa ujenzi wa barabara unajidhihirisha katika barabara za Zanzibar zilizojengwa kwa utaalamu huo- Karakana Mwembe Makumbi, Fuoni Kwarara, Kisasi Junction, maeneo ya Kambi ya Jeshi, Saateni Shaurimoyo, Kibweni zote zikiwa Unguja na pia eneo la Mgagadu, Pemba.

Malambi anasema kuwa, ujenzi wa barabara hizo ulianza kwa njia ya majaribio na tayari uimara wake umethibitishwa, huku gharama zake zikitambuliwa kuwa ndogo kulinganisha na matumizi ya teknolojia ya kawaida.

Anasema ujenzi wa barabara hizo hupunguza zaidi ya asilimia 80 ya muda wa kawaida wa ujenzi wa barabara za lami, hivyo kuokoa muda zaidi kwa shughuli zingine.

``Katika matumizi ya lami, kuni pia hutumika kuilainisha kabla ya kuanza kuwekwa barabarani, hatua hiyo huzalisha moshi mzito ambao huvuruga utando wa hewa iliyopo,`` anasema Malambi.

Utaalamu huo wa kisasa ni muhimu kwa serikali ya Tanzania kwa sasa, ikiwa inahitaji kuona maisha bora kwa kila Mtanzania.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.