09 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Watoto waliokwenda India kutibiwa moyo warejea
 
2008-05-09 08:57:50
Na Joseph Mwendapole

Watoto 26 waliokwenda nchini India kwa matibabu ya moyo katika hospitali ya Narayana Hrudayalaya, wamerejea nchini wakiwa na afya njema baada ya kufanyiwa upasuaji.

Waliwasili jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kupokelewa na viongozi wa Lions Klabu ya Dar es Salaam (Host).

Daktari aliyeambatana na watoto hao, Dk. Ali Amour, alisema watoto wote wako katika hali nzuri tofauti kabisa na walivyokuwa kabla ya kufanyiwa upasuaji.

Alisema wengine hawakuwa na uwezo hata wa kutembea lakini baada ya upasuaji wanaweza hata kukimbia.

Mmoja wa watoto hao, Rajab Hussein, alisema awali hana uwezo hata wa kutembea kwani alikuwa anachoka sana.

Alisema baada ya upasuaji hali imekuwa tofauti kabisa kwani ana uwezo wa kufanya mambo ambayo hakuweza kuyafanya awali.

Mwingine Amina Elias (18), alisema amekuwa akiishi kwa maumivu makali kwa muda mrefu na kwamba anapata shida sana wakati wa kupumua.

Lakini baada ya upasuaji alisema hali yake imetengemaa na anapumua vizuri.

Mama wa mtoto Aftah Salehe, alisema mtoto wake alikuwa na matatizo ya kubadilika rangi mara kwa mara kutokana na kuwa na tundu kwenye moyo.

Alisema awali hakuwa anaweza kutembea lakini baada ya upasuaji anatembea na kucheza na wenzake kama kawaida.

Kijana mwingine Ayubu Isamila (18), alisema alikuwa na tatizo la Valvu mbili ambazo madaktari walisema hazifanyi kazi.

Kwa mujibu wa Daktari wa Hospitali ya Regency, Dk. Rajni Kanabar, madaktari waliomtibu walisema uhai wa kijana huyo uko mashakani lakini kwa mapenzi ya Mungu amepona.

Dk. Kanabar alisema kijana huyo alikaa katika chumba cha watu mahututi (ICU) kwa muda wa mwezi mmoja akipatiwa matibabu.

Alisema kwa kawaida tiba ya aina hiyo hugharimu Dola 24,000 za Marekani lakini hospitali ya Narayana hrudayalaya iliyoko mji wa Bangarole India ilitoa punguzo kubwa.

Dk. Kanabar aliongeza kuwa mtoto mmoja Elizabeth Malindi (4), kutoka Zanzibar alifariki kabla ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.