09 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Waliobomolewa Tabata leo kung`olewa kwa nguvu
 
2008-05-09 08:59:13
Na Simon Mhina

Kampuni ya Allied Cargo Freighters ambao ni wamiliki halali wa eneo la Tabata Dampo, leo imeahidi kuingia na kulitwaa eneo lao baada ya wakazi waliobomolewa nyumba zao kulipwa fidia ya Sh. milioni 20 kila mmoja.

Kwa mujibu wa msimamizi Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. John Nyange, tayari wameteua kampuni ya Majembe Auction Mart kwa ajili ya kuwasambaratisha wakazi hao aliowaita wakaidi na kwamba wamepeleka maombi ya kuomba ulinzi polisi.

Bw. Nyange aliishutumu serikali kwa madai ya kuwabeba wananchi hao na kupuuza haki za kampuni hiyo na kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abbas Kandoro, aondoe mahema aliyowajengea eneo hilo.

Hata hivyo, akionekana kuchukizwa na kauli hiyo, Bw. Kandoro alisema kampuni hiyo haina ubavu wa kumpa amri kwamba aondoe mahema aliyowapa wakazi hao ili wajisitiri baada ya kubomolewa nyumba zao.

``Hawana ubavu wa kunipa amri mimi, tena iwe mwanzo na mwisho, wasirudie! Mimi anayetakiwa kunipa amri ni Rais, Makamu wake au Waziri Mkuu na si vinginevyo,`` alisema Bw. Kandoro.

Alisema kampuni hiyo haina sababu yoyote ya kuharibu mchakato wa kumaliza tatizo hilo, ambao umefikia ukingoni.

Alisema baada ya wakazi hao kulipwa, kinachosubiriwa sasa ni kupatiwa hati za viwanja walivyopewa eneo la Buyuni na vibali vya ujenzi.

``Sasa hawa wanaponiamrisha eti niondoe maturubai yangu, kwanza ni kebehi, lakini pia wanajaribu kuvuruga jambo hilo ambalo kimsingi tumeshalimaliza kwa amani, maelewano na uaminifu mkubwa,`` alisema.

Naye Meya wa Manispaa ya Ilala, Mstahiki Abuu Jumaa alionyesha kusikitishwa na madai ya kampuni hiyo na kuwataka viongozi wake wavute subira.

Bw. Jumaa alisema hatua yoyote ya kampuni hiyo kuvamia eneo hilo kwa pupa, itaharibu utaratibu mzima ambao unakaribia kukamilika, ili wakazi hao wahame.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Bw. Faustine Shilogile alisema maombi ya kampuni hiyo kuomba ulinzi hayajawafikia, lakini akasisitiza kuyapinga kabla hayajafika.

``Hilo la kuhamisha watu halituhusu, hatuwezi kupeleka askari wetu huko, sisi tunafanya kazi kwa utaratibu,`` alisema.

Wakati hayo yanaendelea,wakazi hao wameonya kampuni hiyo kwamba watapata kipigo cha mwaka iwapo watasisitiza kutwaa eneo hilo.

Kiongozi wa wakazi hao Bw. Tauzeni Hariri alionya kwamba wao ni watu wa amani, na ndio maana walikuwa kimya baada ya kubomolewa nyumba zao kwa makosa.

Naye Mwenyekiti wa wahanga hao Bw. Said Masoud, alisema bado kesi ya msingi kuhusu nani mmiliki halali wa eneo hilo, ipo mahakamani.

Alionya kuwa kuwaondoa kwa nguvu ni kuingilia uhuru wa mahakama kutoa maamuzi halali.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.