|
Abambwa akisafirisha wahamiaji haramu
2008-05-09 09:01:58
Na Idda Mushi, PST, Morogoro
Mkazi wa Himo Moshi Mkoani Kilimanjaro, William Makina (34), amekamatwa wa polisi mkoani Morogoro baada ya kukutwa akisafirisha raia 34 wa Somalia ambao hawakuwa na vibali vya kuingia wala kuishi nchini.
Taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Bw. Thobias Andengenye, zilisema Makina, alikamatwa jana, saa 5: 30 na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani katika eneo la Dumila wilayani Kilosa, katika barabara kuu ya Morogoro-Dodoma.
Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akiendesha lori aina ya Fuso namba T 315 ADM lililokuwa likitokea Kiteto mkoani Manyara kuelekea jijini Dar es Salaam na kwamba dereva huyo na raia hao wa Kisomali watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za upelelezi kukamilika.
Taarifa zaidi zilidai kuwa raia hao walikuwa wakielekea nchi za nje, ikiwemo Malawi kupitia Dar es Salaam na walikodi gari hiyo kwa gharama ya sh. milioni moja.
Wakati huo huo, wakazi wawili wa Dakawa na Magole wilayani Kilosa, Ibrahim Habibu (50) na Hamis Mohamed (35) mwenye asili ya Kiarabu, walikamatwa katika eneo la Kitete kata ya Dumila tarafa ya Magole, wilayani Kilosa, wakiwa na bunduki aina ya Shortgun yenye mitutu miwili bila kibali cha kumiliki silaha hiyo.
Kamanda Andengenye, alisema watuhumiwa hao walikamatwa na askari wa Jeshi la Ulinzi, Sajenti Thobias Meicho na Juma Machangu, wakiwa wameifunga bunduki hiyo yenye namba 41987 kwenye mfuko wa sandarusi wakielekea kijiji cha Mvumi wilayani Kilosa.
|