|
Msiwanunie CCM - CUF
2008-05-09 09:05:47
Na Richard Makore
Chama cha Wananchi (CUF), kimewataka wafuasi wake kuacha kununiana na kutoshirikiana na wananchama wa CCM kama hatua ya kujenga mazingira mazuri ya mazungumzo ya Mwafaka visiwani Zanzibar.
Wafuasi wa CUF hivi sasa hawasalimiani wala kushirikiana katika shughuli zozote za kijamii na wenzao wa CCM.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alikiri kuwepo kwa hali hiyo huko visiwani Zanzibar.
Profesa Lipumba, alisema wafuasi wake wamefikia hatua hiyo baada ya kuamini kwamba CCM wamekwepa kusaini makubaliano ya Mwafaka yaliyoendeshwa na vyama hivyo.
Profesa Lipumba, alisema mazungumzo ya kutafuta Mwafaka yasiposainiwa haraka hali hiyo inaweza kuwa kubwa kuzidi ile ya mwaka 2001 baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.
Alisema wanachama wake wamekuwa wavumilivu kwa muda mrefu huku viongozi wao wakiendelea kuwasihi wawe watulivu lakini CCM wamekuwa kigeugeu.
Aliongeza kuwa hata wananchi wengine ambao sio wanachama wa CUF wamechoka na ujanja unaoendelea kufanywa na CCM katika kukwepa kusaini mazungumzo hayo.
Profesa Lipumba, alisema mwaka 1995 baada ya uchaguzi hali pia ilikuwa mbaya lakini wakatumia busara kuwasihi wafuasi wao wajiingize katika vurugu.
Alisema imefikia hatua sasa wanaulizwa na wanachama wao kwamba mbona wamekuwa wakiwadanganya miaka yote kuwa mazungumzo ya kutafuta Mwafaka yatafikiwa.
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyokutana huko Butiama mkoani Mara mwezi uliopita ilikuabaliana kwamba suala la kutafuta Mwafaka Zanzibar lilirudishwe kwa wananchi.
Wakati huo huo, CUF kimesema hakiamini kama kauli ya CHADEMA kwamba haikiungi mkono kuhusu ombi lao la kutaka iundwe serikali ya mseto huko visiwani lilitolewa na chama rasmi.
Profesa Lipumba alisema, Mwenyekiti wa CHADEMA Bw. Freeman Mbowe na Katibu wake Dk. Wilbrod Slaa, hawajawahi kuwaambia suala hilo.
Wiki hii Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Chacha Wangwe, aliwaambia waandishi wa habari kwamba chama chake hakiungi mkono CUF kulilia kuundwa kwa serikali ya mseto huko Zanzibar.
Bw. Wangwe alisema, CUF wanachotakiwa kufanya ni kukazana ili hatimaye wakiondoe CCM madarakani na sio kuomba kushirikishwa katika serikali ya mseto na chama hicho.
Wakati huo huo, Mashaka Mgeta anaripoti kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), `kimewaangukia` viongozi wa dini na kuwataka waeleze ukweli kuhusu mazungumzo ya mwafaka wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yussuf Makamba, alipokuwa akizungumza na wananchi mjini Singida.
Bw. Makamba, alisimama kwa muda mjini humo, wakati akiwa njiani kuekelea mkoani Kagera ambapo atafanya ziara ya siku mbili.
Taarifa iliyotolewa jana na ofisi ndogo ya CCM jijini Dar es Salaam, ilimkariri Bw. Makamba, akiishutumu CUF, kwa kupotosha kuhusu hatua iliyofikiwa katika mazungumzo kati ya vyama hivyo kuhusu mwafaka huo.
\"Katibu Mkuu huyo wa CCM, alisema ajenda za mazungumzo hayo zilikuwa tano, na kwamba hadi sasa, zimezungumzwa nne na kubaki moja, ambazo hata hivyo hazikutajwa.
``Kwa msingi hiyo, amesema ni upotoshaji kusema CCM inakataa kusaini makubaliano wakati inaeleweka ajenda zenyewe hazijamalizika na makubaliano kuhusu ajenda zote hayajakamilika,`` taarifa hiyo ilieleza.
Aidha, taarifa hiyo, ilieleza kuwa Bw. Makamba, aliyaomba makundi ya kijamii wakiwemo viongozi wa dini na wazee, wauelewe vizuri ukweli huo na wasaidie kuueleza kwa wananchi.
Bw. Makamba, alisema dhamira ya CCM ni kuendelea na mazungumzo hadi mwafaka utakapopatikana kwa maslahi ya Taifa.
Alisema dhamira hiyo ipo pia kwa Rais Jakaya Kikwete, kama alivyosema Desemba 25, 2005 wakati akilihutubia Bunge mjini Dodoma.
|