|
Simba wamsimamisha Kaduguda
2008-05-14 09:49:15
By Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu wa klabu ya soka ya Simba, Mwina Kaduguda amesimamishwa kwa muda usiojulikana kwa utovu wa nidhamu na kamati ya utendaji ya klabu hiyo iliyokutana juzi.
Habari za kuaminika toka ndani ya klabu hiyo na kuthibitishwa na mmoja wa viongozi wa klabu hiyo zinasema kuwa, Kaduguda amesimamishwa na kikao hicho cha dharura kufuatia kitendo chake cha kumkashfu mfadhili wao mkuu.
Wajumbe wa kamati ya utendaji chini ya Mwenyekiti wake, Hassani Dalali wamedaiwa kufikia uamuzi kwa kinachodaiwa kushindwa kuendelea kuvumilia tabia za katibu mkuu wao huyo kwa muda mrefu.
Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa, kwa muda mrefu katibu huyo amekuwa `akiharibu` lakini wenzake walikuwa wakimvumilia na kwa kitendo cha juzi cha `kumghasi` na kumkera mfadhili huyo wenzake wameamua kumgeuka.
``Yapo mambo mengi ukiambiwa yanafanywa na kiongozi huyu msomi huwezi kuamini, lakini wenzake wamekerwa na kuamua kumtia adabu, hadi hapo atakapoitwa kwenye mkutano mkuu ili kujitetea kwa adhabu aliyopewa,`` chanzo hicho kilisema.
Nipashe lilimtafuta mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, ambaye alikiri kuwepo kwa maamuzi hayo, lakini akisema yalikuwa bado ayajabarikiwa mpaka kwanza kikao hicho kilichokuwa kikiendelea kimalizike.
``Ni kweli tunakutana hivi sasa kwa kikao cha dharura na moja ya maamuzi ni kumjadili katibu wetu, lakini ukweli ni kwamba huenda tukamsimamisha kwa muda hadi hapo atakapojitetea kwa nini asifukwe uongozini,`` kiongozi huyo (jina na cheo chake tunalo) alisema.
Kiongozi huyo, alisema kuwa tangu walipoingia madarakani Desemba 3, mwaka juzi, katibu mkuu wao huyo amekuwa akifanya mambo ya ajabu, lakini walikuwa wakimvumilia kwa ajili ya kuepusha matatizo klabuni, lakini uvumilivu wao umefikia kikomo.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa msimamo wake wa mrengo wa kushoto wa katibu huyo dhidi ya wafadhili wa klabu ndiko kunakoifanya Simba isisaidiwe kama suala la kulipwa kocha lililokuwa likifanywa na mfadhili aliyefanyiwa fujo na kupelekea viongozi wa klabu hiyo kutaka kumpiga Kaduguda kwa hasira.
Mwandishi wa habari hizi alijaribu kumsaka Kaduguda ili kupata maelezo yake juu ya taarifa hizo za kusimamishwa kwake, lakini hakuweza kupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuzimwa.
|