|
Usuluhishi nje ya mahakama uhimizwe
2008-05-14 10:18:12
Na Mhariri
Misongamano mikubwa ya kesi katika mahakama za ngazi mbalimbali nchini, imekuwa ni moja ya kero ambazo zinazidi kuwanyima haki za kimsingi baadhi ya watuhumiwa.
Suala la mtuhumiwa kupata fursa ya shauri lake kusikilizwa haraka baada ya kufikishwa mahakamani, ni haki yake hadi pale ambapo labda atatiwa hatiani na kuhukumiwa.
Imekuwa ni faraja kubwa juzi kumsikia Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani akiwaagiza mahakimu na mawakili, kushirikiana katika kuwashauri wananchi kumaliza baadhi ya migogoro nje ya mahakama.
Jaji Ramadhani alitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua semina ya mawakili kuhusu utatuzi mbadala wa migogoro ya kisheria nje ya utaratibu wa kimahakama, iliyohudhuriwa na wadau wa sheria wakiwamo mahakimu na mawakili.
``Sheria inayoruhusu utatuzi wa migogoro nje ya utaratibu rasmi wa kimahakama ipo, itumieni vizuri ili kupunguza misongamano ya kesi mahakamani.
``Zipo kesi zenye uzito, ambazo zinapaswa kuingizwa katika utaratibu rasmi, lakini si mashauri yote, mengine yanaweza kumalizwa nje ya utaratibu huo,`` alisema Jaji Ramadhani.
Hakika, baadhi ya migogoro, mathalani inayohusiana na matusi ya nguoni, kuua kwa maneno, mipaka ya ardhi, uhasama wa kifamilia na kadhalika, inaweza kumalizwa nje ya mahakama endapo panakuwepo na usimamizi madhubuti.
Zipo baadhi ya kesi ambazo badala yake hubaki kuonekana kama michezo ya kuigiza mahakamani kutokana na kutokuwa na uzito au wafunguaji wa kesi hizo kufanya masihara.
Tungependa kutoa wito kwa waendesha mashtaka kuwa makini zaidi kuchuja kesi ambazo zina uzito wa kusikilizwa kwa utaratibu wa kimahakama ili kuweza kupunguza misongamano.
Imezoeleka kuibuka tabia ambapo kila mwananchi anayehisi kunyimwa haki kukimbilia polisi na baadaye mahakamani hata kama kesi yenyewe inahusu wizi wa kuku.
Lazima tufikie mahali tukubali kwamba, endapo mahakama za Tanzania hazitabadilika kudhibiti kuibuka kwa kesi za kipuuzi mahakamani, watuhumiwa wengi wataendelea kusota rumande kwa vipindi virefu pasipo ulazima.
Upunguzaji misongamano ya kesi mahakamani iwezeshe kuundwa kwa mahakama maalumu kwa tuhuma ndogo ndogo kama za uzembe na uzururaji au kukutwa na misokoto ya mihadarati kama ya bangi.
Kesi kama hizo ambazo hazihitaji uchunguzi, zinaweza kumalizwa haraka kama ilivyo kwa mahakama za manispaa mbalimbali mijini.
Wananchi nao wanastahili kuheshimu sheria mbalimbali ili kuweza kupunguza migogoro ndani ya jamii.
Usuluhishi nje ya mahakama kwa baadhi ya kesi, siyo tu utazipunguzia mahakama mzigo, bali pia utawapa fursa wahusika kuweza kuokoa muda mrefu ambao ungeweza kupotezwa mahakamani.
Hata hivyo, migogoro hii inayomalizwa nje ya mahakama, izingatie haki za kisheria kwa pande zote zinazohusika.
|