14 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Watanzania wahimizwa kuendesha mitandao
 
2008-05-14 10:21:03
Na Joseph Mwendapole

Serikali imesema ni aibu na hatari anuani za mtandao za Tanzania kumilikiwa na kuendeshwa na wageni. Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Dk. Naoni Katunzi, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo, Bw. Jeremiah Sendoro.

Alikuwa akizindua taasisi ya kusajili anuani za mtandao iitwayo Tanzania Network Information Center (tzNic).

Alisema inashangaza kuona huduma za anuani za mtandao zinazohusu Tanzania kama (dot tz) zinaendeshwa na raia wa Marekani aitwaye Bw. Randy Bush.

``Nimekuwa nikijiuliza kwa nini hawa wageni wamiliki raslimali zetu, kwani hatuna uwezo wa kitaalamu kusimamia hizo anuani,`` alisema na kuongeza kuwa ni wakati muafaka kwa Watanzania kuamka na kusimamia wenyewe rasilimali zao.

Alisema kama Tanzania inataka kufaidika na teknolojia katika masuala ya kijamii, uchumi na kiusalama ni vyema anuani za dot tz zikamilikiwa na Watanzania wenyewe.
Alisema uzoefu duniani kote unaonyesha kuwa ili wananchi watumie anuani zao kwa ufasaha lazima kiundwe chombo cha kusimamia anuani hizo.

Alisema taasisi ya tzNic imeanzishwa kwa ajili ya kusimamia anuani hizo na aliiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA na Umoja wa Watoa Huduma za Mtandao, TISPA kusaidia taasisi hiyo ili iweze kutimiza malengo yake kama ilivyokusudiwa.

Dk. Katunzi, alisema kuna changamoto kubwa kwa wadau kubuni na kuendeleza huduma na vifaa vinavyoweza kutumiwa na Watanzania walio wengi.

Alisema mazingira ya sasa yanatoa fursa kwa wadau kushirikiana na serikali katika kuondoa vikwazo vya maendeleo ya teknolojia hapa nchini.

Aliongeza kuwa teknolojia imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na utoaji wa huduma mbalimbali.
``Tutumie wiki hii kuimarisha ushirikiano na ubia baina ya wadau wa sekta hii katika kufikia malengo ya fursa za TEKNOHAMA,`` alisisitiza.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.