|
Magufuli aagizwa kuchunguza sababu za mapato kidogo Ziwa Victoria
2008-05-14 10:26:29
Na Mwandishi wa PST, Mwanza
Rais Jakaya Kikwete amemwagiza Waziri wa Wizara ya Maendeleo na Mifugo na Uvuvi, Bw. John Magufuli kuunda kamati (task force) itakayochunguza sababu za Tanzania kupata mapato kidogo kutokana na mazao ya Ziwa Victoria ukilinganisha na Kenya na Uganda.
Rais aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza minofu ya samaki cha Tanzania Fisheries Development Company (TFBC), jijini Mwanza jana.
Alisema mwaka jana Tanzania ilipata Sh. bilioni 197.7 kutokana na minofu ya samaki, wakati nchi jirani zilipata Sh. bilioni 202.
``Ukiangalia jirani zetu wana eneo dogo lakini zinapata mapato makubwa ukilinganisha na Tanzania.
Hiyo kamati itatakiwa kuchunguza ili kujua uzembe uko wapi katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kuangalia namna ya kudhibiti utoroshaji wa samaki nje ya mipaka yetu.
Rais Kikwete alisema kuna kila dalili kuwa samaki wengi wanapelekwa nje ya nchi kimagendo hali ambayo inaisababishia nchi hasara kubwa.
Alisema Jiji la Mwanza lina viwanda 12 vya minofu ya samaki ukilinganisha na Bahari ya Hindi ambayo ina viwanda vidogo tena vitatu tu.
Alisema uvuvi haramu ni lazima ukomeshwe kwa nguvu zote na wavuvi waache kutumia makokoro, nyavu za nchi tano na baruti.
Aidha, alizishauri nchi za Kenya, Uganda na Tanzania zishirikiane katika kupambana na uvuvi haramu na lisiwe ni jukumu la nchi moja kukabiliana na vita hivyo.
Alimtaka waziri Magufuli kuhakikisha kuwa wizara yake inaanzisha miradi ya kufuga samaki nchini kote kama ilivyo katika nchi za Mashariki ya Mbali kusudi kuwe na uhakika wa soko la samaki badala ya kutegemea maziwa na bahari pekee.
Aliwapongeza NICO kwa kuwa wazawa na kusema kuwa anategemea kuwa menejimenti ya kiwanda hicho itawajali wazawa ili kiwe kiwanda bora cha mfano katika viwanda vyote vya samaki nchini kwa kuhakikisha ubora wa minofu ya samaki unakuwa wa kiwango cha kimataifa.
Aidha, alisema NICO iimarishe uhusiano mzuri na wavuvi ambao tayari umeanza na kwamba serikali itaendelea kushirikiana na NICO katika kuendeleza miradi mbalimbali ambayo wameianzisha.
Naye waziri Magufuli alisema samaki aina ya sangara wanazidi kupungua katika Ziwa Victoria kwa sababu ya uvuvi usio endelevu.
``Miaka ya nyuma kulikuwa na tani milioni mbili za sangara, utafiti uliofanywa mwaka 2006 unaonyesha kuwa kuna tani 750,000 za sangara, na utafiti wa mwaka huu unaonyesha kuna tani 375,000. Yote haya yanasababishwa na uvuvi haramu, makokoro na mitego midogo,`` alisema.
Hata hivyo, aliipongeza NICO kwa kuweka uwazi katika kupima samaki, jambo ambalo viwanda vingine vimekuwa havifanyi.
Alisema wakiendelea na utaratibu huo utasaidia kuondoa malalamiko ya wavuvi ya kudhulumiwa samaki wao maana viwanda vingine vilikuwa haviwapi fursa ya kuangalia samaki yupi anafaa na yupi hafai.
Naye Mwenyekiti wa NICO, Bw. Felix Mosha, alisema kuwa kiwanda hicho kimegharimu Sh. bilioni 5.2 na kitatoa ajira kwa Watanzania 600, ajira zisizo rasmi 2,000 na kwamba ni kiwanda cha kisasa kuliko viwanda vyote vya samaki katika kanda hiyo.
Bw. Mosha alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani 60 za minofu ya samaki na kwamba kwa sasa wameanza kushirikiana vizuri na vyama vya wavuvi ili kuwawezesha wazalendo.
Alisema katika kuhakikisha hilo kutakuwa na mwakilishi wa wavuvi watakaopelekwa kiwandani hapo ili kuhakiki upimaji, na wale walioharibika.
Alisema kuwa hivi sasa NICO ina wanahisa zaidi ya 30,000 na kwamba lengo lao kuwekeza kwenye mazao mengine mbali na samaki, kama vile machinjio ya kisasa ya nyama ya ng`ombe ya kuuza nje na ndani ya nchi, kusindika matunda kwa mikoa mbalimbali inayolima matunda, kutayarisha mbegu bora za mazao na kuanzisha mazao ya kilimo.
Alisema Mei 23, mwaka huu, NICO itaorodheshwa kwenye soko la hisa Dar es Salaam na hisa zake zitaanza kununuliwa.
Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kununua hisa hizo.
|