14 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Barabara za Nangurukuru-Mbwemkuru zakamilika
 
2008-05-14 10:31:01
Na Mwandishi Wetu

Ujenzi wa barabara za Nangurukuru-Mbwemkuru, Mbwemkuru-Lindi-Mingoyo na Mkuranga-Kibiti umekamilika.
Kufuatia kukamilika huko, serikali imesema sasa barabara hizo zinasubiri kufunguliwa.

Taarifa ya serikali iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ikulu jijini Dar es Salaam jana ilisema, ujenzi wa barabara hizo kuu umekamilika kwa kiwango cha lami.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikusema ufunguzi rasmi utafanyika lini na atakayefungua.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, barabara ya Nangurukuru kwenda Mbwemkuru ina urefu wa kilomita 95, Mbwemkuru-Lindi-Mingoyo ina urefu wa kilomita 95 na Mkuranga kwenda Kibiti ina urefu wa kilomita 79.

Ilisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo, ni sehemu ya miradi mikubwa inayojengwa na serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara chini ya Mpango wa Taifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Usafirishaji (TSIP).

Iliongeza kuwa, mpango wa TSIP ni sehemu ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA).
Taarifa ilisema barabara hizo zikifunguliwa, zitaongeza kiasi cha kilomita 269 katika barabara za lami nchini na hivyo kupunguza urefu wa barabara zisizokuwa na lami.

Taarifa ilisema barabara hizo ni sehemu ya barabara kuu tano zilizokuwa zimekamilika kabla ya Rais Jakaya Kikwete kufungua barabara mbili katika siku chache zilizopita.

``Mei 5, 2008 wakati wa ziara yake mkoani Singida, Rais Kikwete alifungua barabara yenye urefu wa kilomita 173 ya Isuna-Singida-Shelui, na juzi akiwa mkoani Mwanza alifungua barabara nyingine mbili,`` ilisema taarifa hiyo.

Iliongeza kuwa, barabara hizo ni ile inayotoka Geita hadi Buzirayombo yenye urefu wa kilomita 100 na Buzirayombo hadi Kyamiorwa yenye urefu wa kilomita 120 ambazo kwa pamoja zinafikisha urefu wa kilomita 393 katika muda usiofikia wiki mbili.

Aidha, iliongeza kuwa, mbali na ufunguzi wa barabara hizo, ujenzi mwingine wa barabara zenye urefu wa kilomita 1,000 unaendelea katika sehemu mbalimbali nchini.

Taarifa ilizitaja baadhi ya barabara hizo kuwa ni Dodoma-Manyoni yenye km 127, Mbeya-Lwanjilo, Marangu-Rombo Mkuu-Mwika-Kilacha, Rombo Mkuu - Tarakea, Tarakea-Rongai-Kamwanga, Ndundu-Somanga, Mwandiga-Manyovu, Arusha-Namanga na Chalinze-Kitumbi.

Ilisema barabara hizo ni mbali na madaraja mawili makubwa ambayo pia ujenzi wake unaendelea. Madaraja hayo ni Daraja la Umoja na Daraja la Ruvu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.