|
CUF yamjia juu Kingunge
2008-05-14 10:32:51
Na Richard Makore
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema Mwenyekiti Mwenza wa Mazungumzo ya Mwafaka, Bw. Kingunge Ngombale-Mwiru, alishindwa kusoma na kuzielewa nyaraka za mazungumzo yao ili kupeleka taarifa sahihi CCM.
Kadhalika, chama hicho kimesisitiza kuwa, agenda zote tano zilizojadiliwa zilikamilika kupitia vikao 21 kwa muda wa miezi 14 ila CCM inaficha ukweli.
Akizungmza katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, aliyekuwa Katibu Mwenza katika mazungumzo ya Mwafaka kutoka CUF, Bw. Ismail Jussa Ladhu, alisema nyaraka zote za mazungumzo hayo wanazo.
Aidha, chama hicho kiligawa kwa waandishi wa habari nakala za nyaraka zote walizojadili na kuzisaini ili kukanusha madai yalitolewa na CCM kwamba, chama hicho kinapotosha umma.
Bw. Ladhu, alisema mtu ambaye CCM ilikuwa ikimuamini bahati mbaya amezeeka na hawezi kusoma na kuelewa kilichokuwa kinazungumzwa.
Kwa upande Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alisema, anashangaa kuona Mahafidhina kumshinda nguvu Rais Jakaya Kikwete, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kilichofanyika Butiama mkoani Mara.
Mahafidhina ni wanachama wa CCM ambao walitishia kujitenga na kujiunga na chama cha Afro- Shiraz Party (ASP) kilichokuwa visiwani Zanzibar kabla ya Mapinduzi mwaka 1964.
Alisema anaamini kwamba Mahafidhina hawakuwa na uwezo wa kuondoka CCM lakini hajui kwa nini Rais Kikwete aliwaogopa.
Aidha, alisisitiza kuwa, chama chake hakitakubali kupokea amri kutoka CCM inayowataka warejee katika meza ya mazungumzo tena.
Alisema hawako tayari kufanya mazungumzo yasiyokuwa na mwisho na kwamba kama imeshindikana kusainiwa walichozungumza Rais Kikwete aingile kati.
Alisema CCM imewazungusha muda mrefu na sasa wamechoka.
``Sisi tumechoka kuzungushwa na wenzetu hawa wa CCM lakini bado nina imani kubwa na Rais kuhusu kuupatia ufumbuzi mpasuko wa kisisa Zanzibar,`` alisema.
Aliongeza kuwa sio kweli CUF kinaupotosha umma na kwamba katika kuthibitisha hilo ni la uongo kimetoa vielelezo vyote kwa waandishi jambo ambalo CCM hakiwezi kufanya.
Bw. Hamad alisema, vielelezo ambavyo ni nyaraka vilisainiwa na wawakilishi kutoka pande mbili katika mazungumzo hayo.
Kuhusu kuunda serikali ya kitaifa visiwani Zanzibar, Bw. Hamad alisema, walikubaliana iundwe mara baada ya mwafaka kusainiwa mwezi Machi mwaka huu.
Alisema walikubaliana pia baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010 iundwe serikali ya mseto itakayokuwa na makamu wa Rais wawili wa kwanza na wa pili.
Bw. Hamad, alisema hakuna ukweli wowote kwamba hawakuzungumzia uundwaji wa serikali ya mseto.
Chama hicho kilisema walijadiliana na CCM na kukubaliana wapendekeze majina ya watu watakokuwa mawaziri katika serikali ya Rais Amani Abeid Karume na nyaraka hizo wanazo.
Aidha, CUF kilikiri kuwa hoja moja ya kutafuta kura za maoni kwa wananchi haikujadiliwa na kuongeza kuwa hiyo ilikuwa nje ya agenda tano za mazungumzo hivyo haiwahusu.
Kwa upande mwingine chama hicho kimekanusha madai kuwa viongozi wake wanatokana na chama cha Hezibola.
Hezibola ni chama cha Waarabu kilichokuwepo visiwani Zanzibar kabla ya Mapinduzi na kwamba wenyewe CCM ndiyo wafuasi na waasisi wa chama hicho akiwemo Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi.
CUF kilitoa mfano mwaka 1963, Mzee Mwinyi aliteuliwa na Hezibola kuwa balozi nje ya nchi lakini wakati akiwa katika maandalizi ya kuondoka nchini kulitokea Mapunduzi ya mwaka 1964 na hivyo akashindwa kwenda.
Vigogo hao wa CCM mwishoni mwa wiki walirudia wito wa kukitaka chama cha CUF kirejee katika meza ya mazungumzo, ombi ambalo linapingwa vikali na chama hicho.
|