14 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Rais asiingiliwe uteuzi wa Mawaziri-Ikulu
 
2008-05-14 10:34:55
Na Mashaka Mgeta

Ikulu jijini Dar es Salaam, imesema Rais Jakaya Kikwete, hapaswi kushinikizwa kuhusu idadi ya mabadiliko anayoyafanya katika Baraza la Mawaziri.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Bw. Salva Rweyemamu, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.

Hivi karibuni, kumeibuka hisia miongoni mwa jamii, huku wakiwepo baadhi ya watu wanaohoji fursa za ufanisi zinazopatikana kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya Baraza hilo.

Rais Kikwete, ameshafanya mabadiliko na uteuzi wa mawaziri mara nne, kutokana na matukio mbalimbali yaliyotokea nchini kwa vipindi tofauti.

Matukio hayo ni pamoja vifo vya waliokuwa Mawaziri, marehemu Juma Akukweti (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu aliyeshughulikia Bunge) na marehemu Salome Mbatia (Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto).

Mabadiliko mengine yalifanywa kutokana na kujiuzulu kwa mawaziri, Bw. Edward Lowassa (Waziri Mkuu), Dk. Ibrahim Msabaha (Afrika Mashariki) na Bw. Nazir Karamagi (Nishati na Madini).

Mawaziri hao walijiuzulu mwaka huu, kutokana na kashfa ya mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura, uliosainiwa kati ya serikali na kampuni ya Richmond.

Aidha, wiki iliyopita, Rais Kikwete ambaye yupo madarakani kwa takribani miaka miwili na nusu sasa, alitangaza Baraza jipya la mawaziri, kufuatia hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge.

Bw. Change, alijiuzulu wadhifa huo kutokana na kashfa ya kuhifadhi dola milioni moha za Kimarekani kwenye benki moja huko Jersey, nchini Uingereza.

``Nadhani tumuache Rais afanye mabadiliko ya mawaziri kwa jinsi anavyoona inafaa, lengo ni kuleta ufanisi na kuwatumikia wananchi…tumpe nafasi afanye kazi zake,`` alisema Bw. Rweyemamu.

Bw. Rweyemamu, alisema mabadiliko yanayofanywa na Rais Kikwete, hayana athari zozote kisheria, kwa vile hakuna kifungu cha Katiba kinachoelezea ukomo wa mabadiliko yanayopaswa kufanywa katika Baraza hilo.

Bw. Rweyemamu, alisema mawaziri waliopo wanapaswa kuungwa mkono kwa vile, pamoja na mambo mengine, wanafanya kazi katika mazingira magumu ambayo hata hivyo, hakuyafafanua.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.