|
Pemba sasa moto
2008-05-14 10:37:32
Na Dunstan Bahai na Mwinyi Sadallah
Watu saba waliokamatwa na polisi usiku wa kuamkia Jumapili kisiwani Pemba, wakituhumiwa kufanya ushawishi wa kisiwa hicho kujitenga, wamefunguliwa mashtaka ya uhaini watakayosomewa mahakamani jijini Dar es Salaam wakati wowote.
Habari za kuaminika kutoka Zanzibar zilizothibitishwa na Ofisa Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar, zilieleza kuwa watuhumiwa hao baada ya kukamatwa walisafirishwa kutoka Pemba hadi Unguja kwa ndege ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Watuhumiwa hao ambao wamegawanywa makundi matatu na kutawanywa kwenye vituo vya polisi vitatu vya Ng`ombe Madema, Mazizini na Ng`ambo ni Salim Mohammed Abeid mkazi wa Mtambile, Mohammed Mussa Ali wa Kiwani na Hidaya Khamis Haji wa Mkoani.
Wengine ni Ahmed Marshed, Khamis Machomane, Mariam Hamad Bakar wote wakazi wa Kichangani Wawi mkoa wa Kusini Pemba, Gharib Omar Ali mkazi wa Wete na Jirani Ali Ahmed wa Micheweni Kaskazini Pemba.
Kwa mujibu wa Ofisa huyo aliyekataa kutajwa jina lake gazetini kwa vile si msemaji wa jeshi hilo, maofisa Usalama wa Taifa na Polisi kutoka Tanzania Bara, walikwenda kisiwani hapo kwa ndege ya JWTZ na kuwakamata watuhumiwa hao na kuwasafirisha usiku huo huo hadi Unguja.
Alisema wakati watuhumiwa hao wanawahoji, walikiri kuwa walifadhiliwa fedha za chakula na kusafiria hadi Umoja wa Mataifa (UN) Dar es Salaam, ambako walikabidhi barua yao ya kutaka kisiwa hicho kijitenge.
Ofisa huyo aliliambia Nipashe kuwa, watuhumiwa hao waliwataja wafadhili na washauri wao wakubwa kuwa ni baadhi ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi.
Akizungumza kwa simu jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Bw. Khamis Mohammed Simba, alisema kuwa kamatakamata hiyo haiwahusu Wapemba tu, kwani mtu yoyote atakayetuhumiwa kujihusisha kwenye kosa hilo atakamatwa popote alipo.
Alisema idadi kamili ya waliokamatwa hadi jana haijafahamika maana kazi hiyo inaendelea na watuhumiwa wamegawanywa na kuhifadhiwa kwenye maeneo matatu tofauti wengine walibakia Pemba, Unguja na Tanzania Bara.
Alipotakiwa kufafanua ni kwa vipi watuhumiwa hao wamegawanywa kwa makundi, alisema inategemea na masuala ya kiusalama zaidi.
``Kwani Mpemba hastahili kuja Bara, kuwaleta huko pia tumezingatia hii ni Jamhuri ya Muungano,`` alisema.
Hata hivyo, alisema ieleweke kuwa msako huo si kwa Pemba tu, kwani mtu yeyote atakayetuhumiwa kushiriki katika kuandaa, kutangaza au kusaidia kwa njia yoyote kufanikisha azma hiyo ya kujitenga, Jeshi la Polisi litamfikia popote alipo.
``Hata wewe tukiambiwa unahusika, tutakufikia popote ulipo. Hili kosa la kujitenga ni kubwa sana linaweza kuhatarisha usalama wa nchi. Jukumu la vyombo vya ulinzi na usalama ni kulinda uhuru na usalama wa mipaka ya nchi yetu,`` alisema.
Kamishna Simba, alisema ni lazima suala hilo lishughulikiwe kwa umakini sana kwani limetishia usalama wa nchi na watu wake.
``Ndugu wa watuhumiwa wasiwe na wasiwasi, wavute subira kwani sheria itachukuwa mkondo wake, itajua nani ni nani na asiye na hatia ataachiwa, wavute subira,`` alisema.
Alivitaka vyombo vya habari kuripoti habari za kweli za kuwaelimisha Watanzania, tofauti na baadhi ya magazeti aliyodai yaliripoti visivyo habari ya kukamatwa kwa Wapemba hao ikiwa ni pamoja na kutaja idadi yao.
Alisema idadi haiwezi kupatikana kwani kamatakamata bado inaendelea ndani ya Pemba na nje.
Hatua ya polisi kuwakamatwa Wapemba inakuja baada ya wananchi 12 wa kisiwa hicho kuwasilisha maombi kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam, kutaka kisiwa hicho kijitenge na kiwe na utawala wake.
Maombi ya wananchi hao yalitaka serikali ya Jamhuri iendelee kuwepo na ya Unguja ijitegemee na Pemba nao wawe na Rais wao.
Hatua hiyo ililaaniwa na baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Bw. Mohammed Seif Khatib, ambaye alisema kitendo hicho ni sawa na uhaini, hivyo wahusika ni lazima wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Baadhi ya viongozi wa serikali walisema visiwa vya Unguja na Pemba katika historia havijawahi kutengana, hivyo wanapotokea watu kutaka kujitenga hawataeleweka kwani kila mtu alivikuta na kuamua kuishi.
|