|
Ilala mbele kwa mbele
2008-05-15 08:49:57
By Jimmy Charles
Wakati Ilala ikiendeleza ubabe kwenye michuano ya kuwania Kombe la Taifa kwa kuichapa Mwanza 3-1, rufaa ya mkoa wa Temeke iliyowasilishwa kwenye Kamati ya Michuano hiyo iliyoundwa na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, juu ya kupinga kutolewa kwenye michuano hiyo na nafasi yao kupewa Mbeya imetupiliwa mbali.
Katika mchezo huo uliokuwa na upinzani wa hali ya juu, Ilala ilijikuta ikicheza pungufu katika muda wa dakika 80 baada ya mchezaji wake Mohamed Banka kupewa kadi nyekundu na mwamuzi Judith Gamba baada ya kutoa lugha chafu.
Pamoja na kuwa pungufu Ilala waliweza kupata bao la kwanza baada ya Musa `Hassan` Mgosi kukosa penati katika dakika ya 16 baada ya kupiga mpira nje ya lango, ambapo katika dakika ya 45 Mgosi alirekebisha makosa yake na kupachika bao baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Athumana Machupa.
Mara baada ya kipindi cha pili kuanza Mwanza walijipanga, ambapo Kocha Mkuu wa timu hiyo John Tegete alifanya mabadiliko yaliyoisaidia timu hiyo, ambapo katika dakika ya 67 Kamana Salim aliisawazishia bao timu yake baada ya kupiga kichwa safi kilichomshinda mlinda mlango wa Ilala Juma Kaseja.
Ilala, ilicharuka zaidi baada ya kurudishwa kwa bao hilo, ambapo katika dakika ya 69 Credo Mwaipopo aliweza kuifungia bao la pili timu yake na baadaye Mohamed Kijuso alikwamisha bao la tatu lililoifanya Ilala itoke kifua mbele kwa ushindi wa 3-1, ambapo sasa itakutana na mshindi wa mchezo wa leo kati ya Pwani na Morogoro katika mchezo wa robo fainali.
Kwa upande mwingine Kamati ya michuano hiyo imeitupilia mbali rufaa ya Temeke baada ya kamati hiyo kuridhishwa na ushahidi kutokana na kuonyeshwa nakala za uhamisho wa kimataifa za wachezaji hao.
|