15 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Msajili kuubana uongozi Simba
 
2008-05-15 08:51:11
By Badru Kimwaga

Uongozi wa klabu ya soka ya Simba unatarajiwa kuwekwa `kitimoto` na ofisi ya Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo Manispaa ya Ilala, ili kueleza sababu zinazowafanya washindwe kuitisha Mkutano Mkuu wa wanachama katika muda unaotakiwa.

Msajili wa vyama wa Ilala, Penina Maduhu alisema jana kuwa, pamoja na ukweli kuwa ofisi yao haijapata malalamiko rasmi toka kwa wanachama juu ya kucheleweshwa kwa mkutano huo, lakini watawaita viongozi wa Simba kutaka kujua kitu gani kinawakwaza wasiuitishe hadi leo hii.

Maduhu alisema kwa mujibu wa Katiba ya Simba mkutano huo ulipaswa kufanyika siku nyingi, lakini hajui kuna lipi linaloendelea na ndio maana wameamua kuchukua hatua ya kuwaita viongozi wa klabu hiyo kujua kulikoni.

``Tutawaita na kutaka watueleze imekuwaje hadi leo hii mkutano huo umekuwa ukipigwa danadana na kusikiliza sababu zao kama ni za msingi, lakini ukweli mkutano ulipaswa kuitishwa kitambo na wanaoudai wana haki kikatiba,`` Msajili huyo alisema.

Alisema kuwa siku zote ofisi yake imekuwa ikipigishana kelele na kuzisisitizia klabu na vyama juu ya kuzingatia katiba ili kuepusha migogoro na hivyo atakutana na uongozi
wa Simba kuhakikisha mambo yanakuwa sawa.

Aidha, alikanusha madai kwamba amekuwa ikiubeba uongozi wa Simba kwa kukiuka kwa makusudi katiba yao tofauti anavyokuwa mkali kwa wanachama pale wanapoenda kinyume kama kuingilia na kuzima mapinduzi yaliyofanywa mwishoni mwa mwaka jana ya kuung\'oa uongozi wa akina Hassan Dalali.

Kauli ya ofisi hiyo ya msajili imekuja wiki moja tu baada ya baadhi ya wanachama kuushinikiza uongozi wao kuitisha mkutano huo mwezi huu kama ahadi yao huku wakiitupia lawama ofisi ya msajili huyo kuwa ukimya wake ni kubariki kuvunjwa kwa Katiba ya Simba.

Tayari uongozi wa Simba, umeshanukuliwa ukisema kuwa ni ndoto mkutano huo kufanyika mwezi huu kuwataka wanachama watulie hadi Juni utakapoitishwa kupisha zoezi la ugawaji wa kadi mpya za wanachama.

Awali, mkutano huo ulikuwa ufanyike Desemba mwaka jana na kusogezwa mbele hadi Februari mwaka huu lakini ukashindikana kufanyika kwa maelezo ya kupishwa kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu na ndipo hivi karibuni ukaibuka na kusema utafanyika Juni katika tarehe itakayopangwa na kikao cha Kamati ya Utendaji.

Wakati huohuo, msajili wa Vyama na Klabu za Michezo Manispaa ya Ilala, Penina Maduhu amesema kuwa ofisi yake bado haijapata taarifa rasmi juu ya kusimamishwa uongozi kwa Katibu Mkuu wa Simba, Mwina Kaduguda na hivyo hawezi kusema lolote kwa sasa kuhusu maamuzi hayo.

Hata hivyo msajili huyo amesema iwapo, maamuzi hayo yatakuwa yamezingatia katiba ya klabu hiyo ofisi yake haitakuwa na neno zaidi ya kuyabariki kwa kuamini demokrasia imetumika.

  • SOURCE: Nipashe
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.