|
Michango haramu ikomeshwe mashuleni
2008-05-15 08:58:21
Na Mhariri
Kumezuka tabia ambayo inazidi kukomaa katika shule mbalimbali za msingi na za sekondari nchini ambapo walimu huwachangisha wanafunzi fedha pasipo utaratibu unaoeleweka.
Vipo visingizio vingi kama vile kuchangia mitihani mbalimbali ya majaribio, karatasi, kulipia picha, ujenzi ama tai.
Katika hali ya kusikitisha, zipo taarifa kwamba baadhi ya shule hufikia hadi kuwaadhibu ama kuwaondoa madarasani wanafunzi ambao hushindwa kulipa fedha za mitihani hiyo ama michango mengine inayotungwa na walimu.
Jana katika gazeti hili tulichapisha barua ya mzazi ambaye alikuwa analalamikia Shule za Msingi za Minazi Mirefu na Airwing, zilizoko katika Kata ya Ukonga jijini Dar es Salaam kwa kuwachangisha wazazi michango isiyokwisha.
Baada ya kuchapisha barua hiyo, tulipigiwa simu na wazazi kadhaa wakielezea kuiunga mkono na kueleza kwamba hata katika baadhi ya shule nyingine jijini Dar es Salaam ambako watoto wao wanasoma, tatizo la michango ya ghafla na ya kila mara limekuwa sugu.
Mzazi mmoja alitoa mfano wa Shule ya Sekondari ya Nurulyakini, iliyoko Tandika, Dar es Salaam kwamba hivi karibuni ilizua mchango wa kulazimisha wanafunzi kununua tai hapo shuleni, bila kuwaarifu wazazi kwanza.
Alisema kinachowasikitisha ni hatua ya shule hiyo kuwazuia hata wanafunzi wa kidato cha nne kuingia madarasani kwa sababu hawajalipia hiyo tai, licha ya kwamba wanakabiliwa na mitihani ya majaribio siku chache zijazo.
Mbali na michango, yapo pia malalamiko pia ya baadhi ya walimu kupeleka biashara zao ndogondogo mashuleni kama za mayai, karanga, barafu, maandazi, sambusa na kadhalika ambapo huwalazimisha wanafunzi kununua au kuwakopesha kwa lazima.
Tunapokea malalamiko kwamba, baadhi ya wanafunzi ambao huonekana kugoma kununua bidhaa za walimu hao au hata kukopa, hujikuta wakiiingia matatani kwa kujengewa uhasama.
Tunakumbuka kwamba, mara kadhaa, serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imekuwa ikikemea tabia ya baadhi ya walimu kutumia maeneo ya shule kujihusisha na biashara.
Iliilazimu serikali kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini kwamba baadhi ya walimu hudiriki hata kuwalazimisha wanafunzi kutumia muda wa masomo eti kuwauzia biashara zao mashuleni.
Inatusikitisha mno kwamba wakati vilio hivi vya wazazi vikilazimika kuvifikia hadi vyombo vya habari, wenyeviti wa serikali za mitaa, madiwani hata wabunge wa maeneo husika wanaendelea kukaa kimya kama vile hakuna kinachotokea kuhusu kero wanazozipata wananchi hao.
Kibaya zaidi, imegundulika kwamba baadhi ya shule, ikiwemo Sekondari ya Nurulyakini, hazina bodi wala kamati za wazazi ambazo zingeweza kutumika kutafuta njia za kuboresha taaluma na kuongeza kipato cha walimu bila kutumia njia za `kuwalangua` wazazi.
Tunadhani sasa imefikia kipindi ambapo serikali inatakiwa kuwa kali zaidi kuwachukulia hatua walimu wanaopuuza maagizo halali yanayowazuia kuwatoza wanafunzi michango isiyokuwa rasmi.
Sisi tunajua kwamba mitihani ya aina yoyote ile inayofanyika mashuleni lazima iwe katika bajeti zilizotengwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi au pale inapolazimu, kwa testi za kawaida, lazima ipate vibali vya bodi za shule husika.
Kwa shule za binafsi, michango hii lazima ipate baraka za wazazi kupitia vikao na maelezo yanayotosheleza.
Kwa namna yoyote ile, haituingii akilini, walimu kila kukicha kuwabebesha wazazi mzigo wa kuwalipia michango mikubwa isiyo halali watoto wao huku viongozi wa maeneo hayo wakipuuza kuwachukulia hatua.
Tungependa kutoa mapendekezo kwamba kuanzia sasa, walimu watakaobainika kuwatoza wanafunzi michango isiyoidhinishwa na mamlaka husika kama Bodi za Shule, wachukuliwe hatua kali ikiwa ni pamoja na kukatwa sehemu za mishara yao kwa kipindi fulani, kusimamishwa kazi na kama tabia hiyo inajirudia wafukuzwe kazi.
Bodi za Shule nazo tunashauri ziwe zinaitisha mikutano inayowashirikisha wazazi, walau mara mbili kila mwaka ili kujadili kwa pamoja mambo yanayolazimu kuwepo michango yenye lengo la kuboresha elimu kwenye shule husika.
|