|
Nani zaidi? FM Academia au Akudo
2008-05-16 09:18:11
By Sabato Kasika
Mwanamuziki mkongwe toka Kongo, Bozi Boziana ambaye kwa sasa jijini Dar es Salaam, amepewa nafasi ya mwisho kutoa burudani kwenye uzinduzi wa albamu ya bendi ya Akudo Impect.
Mratibu wa maandalizi ya uzinduzi huo, King Dodoo, alisema kuwa bendi ya Akudo itasindikizwa na mkongwe huyo pamoja na kundi la Jahazi Modern Taarab.
``Bendi nyingi zimezoea kuzindua kwa kuvitanguliza vikundi vya kusindikiza ndipo bendi rasmi inamalizia, lakini sisi tutafanya kinyume, wataanza Akudo itakuwa na kufuatiwa na Jahazi halafu Bozi Boziana atamalizia,``alisema Dodoo.
Akudo inatarajia kuzindua albamu ya Impact leo usiku, katika ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo imeamua kuibuka kwa staili hiyo ambayo Dodoo amesema ni ngeni kwa mashabiki wengi wa muziki wa dansi ambao wamezoea kuona bendi inayozindua inakuwa ya mwisho.
Baadhi ya nyimbo za albamu hiyo mpya ni Papa Msofe, Safari Siyo Kifo, Mama Vanesa, Yako Wapi Mapenzi na nyingine nyingi.
Wakati huo huo, bendi ya FM Academia `nayo itakuwa na onyesho maalum la sherehe ya kutimiza miaka kumi ambalo leo, katika ukumbi wa New Msasani Club.
Katika onyesho hilo, Mkongwe wa muziki toka Kongo General Deffao atafanya vitu vyake pamoja na kuwalisha keki wale waliozaliwa tarehe kama ya leo ya Mei 16.
Mbali na mkongwe huyo, FM inatarajia kuwashirikisha wanamuziki wote waliowahi kuwa katika bendi hiyo lakini kwa sasa hawapo wako kwenye bendi nyingine ama wameachana na muziki.
Baadhi ya wanamuziki hao ni Ndandaa Kossovo, Chochoto, Malou Stonch, Liva Hassan, Lilian Kinondoni na wengine wengi ambao tayari wamepata mwaliko huo na wamekubali kuhudhuria.
Rais wa bendi hiyo Nyoshi El Sadaat, aliliambia Nipashe kuwa walikuwa wakitamani hata akina Papii Kocha na Nguza Mashine wawepo kwenye sherehe hiyo lakini bahati mbaya taratibu za kuwapata haziruhusu kutokana na matatizo yaliyowakumba ya kupata kifungo cha maisha.
Sherehe hizo pia zitapambwa na kundi la mipasho la New Zanzibar Modern Taarab ambalo lilifufuka hivi karibuni baada ya kukwama kufanya maonyesho kwa miezi kadhaa.
|