|
Taifa Cup yazuia usajili Yanga
2008-05-16 09:20:02
By Somoe Ng`itu
Wachezaji wakongwe wa mabingwa wa soka wa Tanzania Bara, klabu ya Yanga wako katika hatari ya kuachwa katika usajili wa msimu ujao kutokana na baadhi ya wachezaji chipukizi wanaoshiriki katika mashindano ya Safari Lager Taifa Cup kumvutia kocha mkuu wa timu hiyo, Dusan Kondic.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega alisema kuwa Kondic aliwaomba kusitisha kuwapatia orodha ya wachezaji anaowahitaji kutokana na kuvutiwa na baadhi wa wachezaji kwenye mashindano hayo yanayoendelea na kusema kuwa atawasilisha majina kwa viongozi baada ya kumalizika kwa michuano hiyo.
Madega alisema kuwa Kondic aliwaeleza kuwa lengo lake ni kuona kwamba anakuwa na kikosi imara kitakachokuwa tayari kukabiliana na ushindani katika msimu ujao wa ligi na mashindano mengine ya kimataifa.
Madega alisema kuwa hata hivyo kocha wao ameshindwa kuwaeleza ni aina gani ya wachezaji anaotaka kuwasajili na kusisitiza kuwa anahitaji kuangalia vipaji zaidi na uwezo binafsi wa kila mchezaji.
Aliongeza kuwa kocha wao ameshindwa kuweka wazi ni sehemu zipi atahitaji kuwa na wachezaji wapya ambazo hakikufanya vizuri katika msimu uliopita na kusema kuwa hiyo itawekwa wazi baada ya kukamilisha mazungumzo na wachezaji hao.
Mara kadhaa kocha huyo ambaye anatoka Serbia amekaririwa akisema kuwa anahitaji kuwa na makipa wenye uzoefu ambapo hatakuwa na hofu mara mmoja wao atakapokuwa majeruhi.
|