16 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Pwani yaifungisha virago Moro
 
2008-05-16 09:20:55
By Somoe Ng`tu

Timu ya mkoa wa Pwani, Pwani Heroes, jana ilitinga robo fainali kwa matuta baada ya kuichapa Morogoro, Moro Stars, kwa penati 4-2, katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Pwani sasa itakumbana na timu ya mkoa wa Ilala katika mchezo wa robo fainali utakaofanyika wiki ijayo.

Hadi dakika 90 zinamalizika, timu hizo zilikuwa sare ya 1-1 huku bao la Morogoro likiwekwa kimiani na Monja Liseki katika dakika ya 18 baada ya kupokea krosi ndefu iliyochongwa na Idrissa Rajabu.

Pwani inayofundishwa na Fred Felix Minziro iliandika bao la kusawazisha katika dakika moja kabla ya mapumziko kwa bao lililowekwa kimiani na Full Maganga.

Katika mikwaju ya penati Pwani ilipata penati nne zilizowekwa kimiani na Mwinyi Kazimoto, Kessy Mapande, Greyson Haule na Amos Juma, huku wafungaji wa matatu kwa Moro Stars ni Mokili Lambo na Nsa Job wakati Said Mkupi na Nico Kabipe penati zao zilipanguliwa na kipa wa Pwani.

Mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania, TBL, kupitia bia yao ya Safari Lager, yanaendelea tena leo kwa kuzikutanisha timu za Mbeya, Mapinduzi Stars, na majirani zao wa Rukwa.

Mbeya wanacheza hatua hiyo baada ya kushinda rufaa yao iliyosababisha Temeke kutupwa nje ya mashindano hayo yanayoshirikisha timu za mikoa ya Tanzania Bara.

Wakati huohuo, wapenzi wa soka wameufananisha mpambano wa Pwani Heroes na Ilala utakaofanyika Jumatatu sawa na ule wa Yanga na Simba kufuatia kuzikutanisha timu ambazo makocha wao, Fred Felix Minziro wa Pwani mpenzi mkubwa wa Yanga na timu yake hiyo ya mkoa inatumia jezi za njano wakati Temeke inafundishwa na kocha msaidizi wa Simba Jamhuri Kihwelu na timu yake hiyo inavaa jezi zenye rangi nyekundu na nyeupe ambazo hutumiwa na Simba.

  • SOURCE: Nipashe
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.