|
Simba wamshushua Msajili
2008-05-16 09:21:48
By Badru Kimwaga
Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umemruka Msajili wa Vyama na Klabu vya Michezo Manispaa ya Ilala, Penina Maduhu na kudai kuwa hana mamlaka wala uwezo wa kuwaita na kuwahoji kuhusu kutoitisha mkutano wao mkuu kulingana na katiba mpya ya klabu hiyo.
Hata hivyo, uongozi huo wa Simba umewatoa wasiwasi wanachama wake na kuwahakikishia kuwa mkutano huo utafanyika Agosti mwaka huu mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu ujao hii ikiwa ni baada ya kukamilika kwa zoezi la ugawaji wa kadi mpya za wanachama.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassani Dalali alilimbia Nipashe jana kuwa, wanamshangaa msajili huyo kudai atawaita na kuwahoji juu ya kinachowafanya washindwe kuitisha mkutano wao wakati Katiba mpya iliyofanyiwa marekebisho kulingana na maagizo ya FIFA, haiitambua tena serikali.
Dalali alisema kuwa msajili huyo hana jeuri ya kuwahoji juu ya kufanyika ama kutofanyika kwa mikutano ya klabu hiyo kwani kwa sasa katiba yao haimtambui kulingana na mabadiliko ya katiba hiyo iliyopitishwa na Shirikisho la Soka Tanzania, TFF na kubarikiwa na ofisi yake.
Aliongeza kuwa kama kweli msajili angekuwa ni mtu wa kuingilia migogoro na kusuluhisha wangeweza kumrejesha Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, Ismail Aden Rage aliyezuiwa bila sababu za msingi ama kusaidia kumfungulia katibu mkuu wao, Mwina Kaduguda aliposimamishwa na TFF kwa muda wa miezi sita.
Dalali maarufu kama `Field Marshal`, alisema kuwa yeye na wenzake si waoga wa mikutano na ndio maana katika muda wa mwaka mmoja ameitisha jumla ya mikutano mitano kitu ambacho hakijawahi kutokea na kuitaja mikutano hiyo kuwa ni mitatu ya kikatiba na miwili ya dharura.
Mwenyekiti huyo alisema wanachama wanapaswa kutulia na kusubiri zoezi la ugawaji wa kadi likamalizika ili kutoa fursa kwa wanachama wengine kupata uhalali wa kuhudhuria mkutano huo na kusema wametenga muda wa miezi miwili ama mitatu kugawa kadi hizo na kuitisha mkutano Agosti.
Alisema kuwa wanaopiga kelele ya kuutaka mkutano huo ni kwa vile wameshapewa kadi zao na kusema kati ya wanachama 10,000 waliopitishwa kuwa wanachama wapya ni wanachama wasiozidi 500 tu ndio waliogawiwa kadi wengi wao wakiwa ni wanachama wa zamani.
Dalali ametoa ufafanuzi huo kufuatia gazeti hili jana kumnukuu msajili, Penina Maduhu akidai atauita uongozi wa Simba na kuwahoji sababu za kutoitisha mkutano mkuu kama inavyotakiwa na kusisitiza kuwa wanachama wanaoudai wapo sahihi kikatiba.
|