16 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Msimamo wa Ubalozi wa Cuba ni changamoto kubwa
 
2008-05-16 10:01:48
Na Mhariri

Ubalozi wa Cuba nchini uligoma kutoa viza kwa bondia Emilian Patrik kwenda nchini humo kwa mazoezi ya kujiandaa na michezo ya Olimpiki inayofanyika mwaka huu nchini humo.

Cuba ni moja ya vigogo vya mchezo huo duniani, ambapo Emilian angeweza kunufaika na kambi hiyo.
Wacuba ni marafiki zetu wa damu, ambapo kwa ujumla wamekuwa wakiunga mkono jitihada zetu katika kupambana na ujinga, maradhi na umaskini.

Bila shaka, mahusiano hayo yaliimarika zaidi kutokana na uswahiba wa baba wa taifa, hayati mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa kiongozi wa Cuba, Fidel Castro.

Mathalani madaktari wengi wa humu nchini walipata fursa ya kusoma nchini Cuba.

Pia Cuba imetoa mchango mkubwa katika uendelezaji wa sekta ya elimu nchini.

Ipo mifano hai ya shule za sekondari za Kilosa na Ruvu zilizojengwa kwa msaada wa nchi hiyo.

Pia nchi hiyo imetoa msaada mkubwa katika harakati za ukombozi barani Afrika, nani atasahau kipigo cha Cuito Cuanavale nchini Angola, ambapo askari wa UNITA na wale wa Makaburu wa Afrika walichakazwa vibaya.

Kutokana na urafiki huo, Shirikisho la ndondi za ridhaa nchini (BFT) liliomba bondia Emilian Patrick apelekwe nchini humo.

Ubalozi ulitoa maelezo kuwa muda ulikuwa mfupi mno kuweza kumpeka Emilian nchini humo na kuweza kunolewa kisawasawa.

Walishauri kuwa programu hiyo ilitakiwa kufanywa miaka miwili iliyopita na sio sasa.

Ilielezwa kuwa hakuna mantiki kumuandaa bondia kwa michezo mikubwa kama ile ya Olimpiki kwa muda wa mwezi mmoja.

Hili funzo kubwa kutokana na mazoea ya viongozi wa michezo nchini kuandaa wanamichezo wake kwa mtindo wa `zimamoto`.

Takwimu tulizonazo zinatuonyesha kwamba tangu mwaka 1980 Tanzania haijapata medali yoyote katika mashindano ya michezo ya Olimpiki.

Ni bora sasa wamejitokeza watu wa kutuambia ukweli kuwa maandalizi ya `zimamoto` hayawezi kutupatia medali.

Siyo siri kwamba suala hili limekuwa likipigiwa kelele miaka na miaka lakini viongozi wetu wameelekea kuweka pamba `masikioni` mwao.

Imefika wakati kwa viongozi wa michezo kubadilika na kuhakikisha pale michezo ya Olimpiki itakapomalizika mwezi Agosti basi waanze mara moja kuandaa timu ya mwaka 2012.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.