16 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

MEWATA kujenga hospitali maalum ya wanawake
 
2008-05-16 10:05:23
Na Restuta James

Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imetoa Sh. milioni 200 kwa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) kwa ajili ya ujenzi wa hospitali maalum kwa magonjwa ya wanawake.

Kadhalika, WAMA imetoa sidiria 500 maalum kwa wanawake waliokatwa matiti kutokana na ugonjwa wa saratani.

Msaada wa WAMA ulitolewa jijini Dar es Salaam jana na mwenyekiti wa taasisi hiyo, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha afya ya wanawake.

``Tumefanya uamuzi huu ili kutimiza azma ya WAMA kushirikiana na wadau wenzetu kuboresha afya za wanawake na watoto tukitambua wazi kuwa hii ni changamoto inayotukabili katika kufikia lengo kuu la kuboresha maisha ya wanawake na Watanzania kwa ujumla,`` alisema.

Aliitaka MEWATA kupanua huduma zake ili kupambana na changamoto zinazowakabili wanawake.

Mama Kikwete alikishauri chama hicho kuhakikisha kinajenga hospitali yenye sifa na itakayotoa huduma kwa wanawake wengi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa MEWATA, Dk. Florence Temu alisema chama chake kipo katika mchakato wa kuteua mkandarasi na kwamba ujenzi utaanza mara moja pindi zoezi hilo litakapomalizika.

Alisema hospitali hiyo itakapokamilika itaweza kutoa huduma kwa watu wote japokuwa kipaumbele kitakuwa kwa wanawake.

Akizungumzia ukubwa wa tatizo la saratani nchini, Mkurugenzi wa Taasisi ya ugonjwa huo kutoka hospitali ya Ocean Road, Dk. Twalib Ngoma alisema wanawake 8,000 kila mwaka hugundulika kuwa na saratani ya matiti.

Alisema 400 kati yao ndio ambao hubahatika kupatiwa tiba kiasi alichosema ni kidogo.

Aliongeza kuwa asilimia 99 ya wanawake wanaokatwa matiti hukosa vifaa muhimu zikiwemo sidiria maalum jambo linalowaathiri kisaikolojia.

``Tatizo la saratani ya matiti ni kubwa nchini na linaongezeka kila mwaka... labda niwapongeze sana WAMA kwa kutoa sidiria. Msaada waliotoa utakuwa chachu kwa wadau wengine katika kuwasaidia wanawake wenye saratani,`` alisema.

Mama Kikwete alitoa sidiria maalum 200 kwa taasisi hiyo, MEWATA walipatiwa 100 wakati asasi ya kutoa elimu kwa wanawake wenye saratani walipatiwa sidiria 200.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.