16 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kamala awataka wafanyabiashara kujipanga kufanya biashara katika soko la Jumuiya
 
2008-05-16 10:07:17
Na Lusekelo Philemon

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kujipanga vilivyo na kuwa tayari kufanya biashara kwenye soko la pamoja la jumiya hiyo linalotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Dk. Kamala alisema soko la pamoja la jumuiya hiyo, lina fursa nyingi za biashara na masoko kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

``Hivyo ni wakati muafaka sasa kwa wafanyabiashara kuitumia vilivyo fursa hiyo kuweza kujiandaa na kujitupa bila woga kwenye soko hilo ili waweze kujiendeleza kiuchumi,`` alisema waziri Kamala.

Alisema kutokana na umuhimu wa soko hilo, serikali imejipanga vilivyo kuhakikisha kwamba, wafanyabiashara wa Tanzania wanapewa mbinu mbalimbali za kujiimarisha kibiashara.

Moja ya mbinu hizo ni pamoja na kuandaa safari kwa wafanyabiashara ili waweze kutembelea nchi zote zilizomo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema.

``Safari hiyo itafanyika mwishoni mwa mwezi Agosti, mwaka huu,`` alisema Dk. Kamala, na kuongeza kuwa safari hiyo ya kihistoria itawahusisha wafanyabiashara 60.

Alisema wafanyabiashara hao wataweza kutembelea nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda na wataweza kujifunza mambo mbalimbali ya kibiashara ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na wafanyabiashara wenzao katika nchi hizo.

Kwa muujibu wa waziri huyo, safari hiyo itawaongezea uwezo wa kujiamini kwa wafanyabiashara wa Tanzania.

``Hii itawafanya wafanyabiashara wetu waweze kujifunza mbinu mbalimbali za kibiashara na kuingia ubia na wafanyabiashara wenzao wa nchi za Afrika Mashariki,`` alisema Dk. Kamala.

Alisema lengo la serikali ni kuwafanya Watanzania wanufaike na soko la pamoja la jumuiya hiyo.

Pamoja na hilo, Dk. Kamala aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha kuwa wanaandaa maandiko mazuri ya biashara zao na kisha kujiandikisha kushiriki safari hiyo ya kikanda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Dk. Evans Rweikiza alisema ujumbe wa wafanyabishara hao utahusisha wafanyabiashara wenye maandiko mazuri ya biashara na miradi yao.

``Mipango yetu ni kuwafanya wafanyabiashara wetu wanazitumia fursa zote zilizopo na kujiendeleza kiuchumi,`` alisema.

Alisema milango ya kupokea maandiko bado ipo wazi hadi hapo katikati ya mwezi ujao kabla ya kuanza kuyachambua na kuwapata wafanyabiashara watakaokuwa kwenye safari hiyo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.