|
Kortini kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi hadi kufa
2008-05-16 10:09:58
Na Karama Kenyunko
Mfanyabiashara Ngochi Baraka (23), aliyekuwa akishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi hadi kufa, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shtaka la mauaji.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bi. Shamila Kilango alidai mbele ya Hakimu wa Wilaya Bw. Afumwisye Kibona kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 13, mwaka huu, eneo la Kiwalani Yombo, jijini Dar es Salaam.
Ilidaiwa kuwa, siku ya tukio, mshtakiwa alimuua Janeth Kwambaza.
Hata hivyo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Wilaya haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauji na kesi hiyo itatajwa tena Mei 29, mwaka huu.
Wakati huo huo, mkazi wa Sinza, jijini Dar es Salaam, Hassan Ally (34), amefikishwa mahakamani hapo kujibu shtaka la kumnajisi mtoto mwenye umri wa miaka saba.
Mbele ya Hakimu Mkazi Bw. Samwel Maweda, ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bw. Mussa Gumbo kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 8, mwaka huu, eneo la Feri.
Ilidaiwa kuwa, siku ya tukio, mshtakiwa alimnajisi binti mdogo mwenye umri wa miaka saba (jina limehifadhiwa) na kumsababishia maumivu makali mwilini.
Hata hivyo, mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na alirudishwa rumande kwa kukosa wadhamini hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Mei 29, mwaka huu.
Katika kesi nyingine, mfanyabiashara mkazi wa Buguruni Kisiwani, jijini Dar es Salaam, Ally Hashim (29), amefikishwa Mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Bi. Joyce Minde kujibu shtaka la ujambazi wa kutumia silaha.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Mussa Gumbo alidai kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo Aprili 5, mwaka huu, eneo la Buguruni Kisiwani.
Ilidaiwa kuwa, siku ya tukio, mshtakiwa aliiba simu moja ya mkononi yenye thamani ya Sh. 150,000 mali ya Bw. Michael Mbuluma.
Ilidaiwa kuwa, kabla ama baada ya kutenda kosa hilo, mshtakiwa alimtishia mlalamikaji kwa panga ili kuweza kutimiza azma yake hiyo kwa njia rahisi.
Hata hivyo, mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na alirudishwa rumande kwa kuwa makosa ya silaha hayana dhamana na kesi hiyo itatajwa tena Mei 29, mwaka huu.
|