16 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Waziri, waathirika wafanya mkutano chini ya ulinzi
 
2008-05-16 10:13:03
Na Raymond Kaminyoge

Mkutano kati ya Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Kapteni (mstaafu), John Chiligati na wakazi wa Kibamba wilayani Kinondoni kuhusu mgogoro wa ardhi, ulifanyika chini ya ulinzi wa polisi huku wakazi wengine wakizuiwa kutoa malalamiko yao.

Waliozuiwa kutoa malalamiko yao ni wale ambao hawakuruhusiwa kuingia katika ukumbi wa mkutano, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni watetezi wakuu wa wakazi hao akiwemo Mwanasheria, Bw. Chrisant Kibogoyo.

Zoezi la kuwazuia kuingia katika ukumbi wa Urafiki jijini Dar es Salaam jana mahali ulipofanyika mkutano huo lilisimamiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Bw. Jamal Rwambow.

Kufuatia hali hiyo, wakazi hao wa Kibamba walionekana kukasirika na kushindwa kujibu salamu ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kanali Fabian Massawe aliyewasalimia kabla ya kumkaribisha Waziri.

Katika maoni yao kwa Waziri, baadhi ya wakazi hao waliwalalamikia watendaji wa serikali kwa kulipa fidia `majina hewa` huku wamiliki halali wa nyumba na mashamba wakiambulia `patupu`.

``Nyumba yangu na shamba vilifanyiwa tathimini na nikapewa namba 336, lakini nilipokwenda wizarani kuchukua fedha zangu za fidia nikaambiwa zimechukuliwa na mtu aliyetajwa kwa jina la Salum Luoga ambaye hatujui anaishi wapi, hivyo hadi sasa sijalipwa fidia,`` alisema.

Aliongeza kuwa wamefuatilia suala hilo wizarani bila mafanikio hali, ``Mheshimiwa Waziri si pekee yangu, tuko wengi ambao hatujalipwa.``

Bi. Mary Tindwa alimweleza Waziri kuwa fidia aliyopewa ni ndogo ambayo hailingani na thamani halisi ya nyumba na shamba lake.

``Hawa wathamini wa wizara ni watu wa ajabu sana, wamekuja kwangu nyumba iliyoezekwa kwa vigae wao wameandika kuwa ni ya bati, badala yake nimelipwa fedha ambayo haiwezi hata kuniwezesha kununua kiwanja,`` alisema.

Aliomba tathimini ifanywe upya kwa kufuata viwango vya bei ya soko badala ya kulipwa kwa kutumia viwango vya serikali.

Kwa upande wake, Kibogoyo alisema sera ya taifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inaeleza wazi kuwa, serikali itatumia ardhi kama njia muhimu ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Alisema lengo la sera hiyo ni kuwasaidia wananchi watumie ardhi waliyonayo ama kujipatia hisa au pato lenye kuwanufaisha kushiriki kikamilifu katika shughuli zao.

``Sasa kuwahamisha wananchi na kuwalipa fidia isiyolingana na mali zao ni kuwawezesha ama kuwazidishia umaskini, serikali inakwenda kinyume na sera zake yenyewe,`` alisema.
Mkazi mwingine wa Kibamba, Bw. Ahmed Kajilu, alisema kurudia kwa uthamini hakutakuwa na maana ikiwa vitatumika viwango vya serikali.

Alisema inasikitisha kuona fidia waliyolipwa hailingani na bei ya viwanja waliyonunua miaka ya nyuma.

``Shamba unanunua Sh. milioni 1.5 lakini wathamini wa wizara wanakupatia Sh. 700,000, je huko ni kumwezesha mwananchi au kummaliza kabisa,`` alisema.

Eneo la Luguruni na Kibamba kitajengwa Kituo cha Uwekezaji na Uchumi hali inayosababisha wakazi zaidi ya 259 kuhamishwa ili kupisha ujenzi huo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.