|
Kamati ya Muungano heshimuni maazimio-Shein
2008-05-16 10:16:19
Na Mwandishi Wetu
Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, amewaambia Wajumbe wa Kamati ya Masuala ya Muungano kuwa, ni lazima watekeleze na kuheshimu maamuzi, maagizo na maazimio ya kupunguza kero za Muungano watakayoyafikia kwenye vikao vya kamati hiyo.
Akifungua mkutano wa Mawaziri na Wajumbe wa Kamati ya Masuala ya Muungano uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Dk. Shein, aliwaagiza viongozi hao kutekeleza kwa wakati yale wanayokubaliwa na pande mbili hizo za Bara na Visiwani.
Pia alionyesha wasiwasi juu ya muda mfupi uliobakia katika kutekeleza ahadi ya kuondoa kero za Muungano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2010.
Kikao cha Mawaziri wa Kamati ya Muungano kilichofanyika jana ni cha tatu tangu kuundwa kamati hiyo inayoundwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Waziri Mkuu Mkuu, Waziri Kiongozi, mawaziri na wajumbe wengine wa maeneo yaliyo kwenye Muungano.
Alisema muda uliobakia katika kutekeleza ahadi za kuondoa kero za Muungano kama ilivyoanishwa kwenye ilani ya CCM si mrefu na kuwataka wajumbe kuongeza kasi ya kuondoa kero kama CCM ilivyowaahidi wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ya 2005.
Aliwataka kuwa wakweli na wenye dhamira na nia ya dhati ya kuleta ufumbuzi wa matatizo hayo kwa manufaa ya nchi na ustawi wa Muungano.
``Tukumbuke dhamira ya kweli ya serikali zetu ni kuondoa vikwazo vilivyo kwenye Muungano na kuendeleza utamaduni wa kujadili mambo yanayolalamikiwa na kuyapatia utatuzi,`` alisema.
Rais Jakaya Kikwete alitoa maelekezo ya kuundwa Kamati ya Waziri Mkuu pamoja na Waziri Kiongozi na Mawaziri wengine na kuagiza wakutane na kuzungumzia na kutatua matatizo ya Muungano.
Lakini pia alisema sharti kubwa kwenye kutekeleza majukumu yao ni kufuata sheria na kuheshimu katiba za pande mbili za Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Wajumbe wa Kamati ya Muungano waliokuwa kwenye kikao hicho ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano Bw. Mohamed Seif Khatib, Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, Waziri Kiongozi Bw. Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri Kiongozi Bw. Ali Juma Shamuhuna.
Wengine kutoka Zanzibar ni Mawaziri Samia Suluu Hassan wa Utalii, Bi. Asha Abdallah Jumaa, Wanawake, Vijana na Ajira.
Baada ya Makamu wa Rais kufungua kikao hicho, alitoa amri kwa wanahabari kuondoka mara moja ili kutoa fursa kwa wajumbe kuanza mjadala.
Bila ajizi waandishi waliondoka wakionekana kuishangaa hatua hiyo ya `kufukuzwa`.
|