16 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Dk. Slaa aibwaga CCM
 
2008-05-16 10:17:30
Na Charles Ole Ngereza, PST Arusha

Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, imetupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge jimbo la Karatu yaliyompa ushindi ubunge Dk. Wilbroad Slaa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2005.

Kesi hiyo ilifunguliwa na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Karatu wakiongozwa na Joseph Haimu.

Katika shauri hilo walalamikaji waliwakilishwa na mawakili Ezra Mwaluko na Mpaya Kamalla wakati walalamikiwa waliwakilishwa na wakili Tindu Lissu.

Waliofungua kesi hiyo walidai kuwa taratibu za uchaguzi zilivurugwa na msimamizi ikiwemo kutohesabu vizuri kura na kwamba kama zingehesabiwa kwa umakini, mgombea wa CCM, Bw. Patrick Tsere angeibuka mshindi.

Madai mengine ni kuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo hakutangaza matokeo hayo kwa sauti na pia alitangaza wakati matokeo ya baadhi ya kata yakiwa hayajawasilishwa, jambo walilodai katika hati yao ya mashitaka kuwa ni kinyume na sheria.

Pia walikuwa wanadai kuwa wakati wa zoezi la kutangaza hakukuwepo na ulinzi na kwamba matokeo yalitangazwa wakati mgombe wa CCM akiwa hayupo, hali waliyodai ilionyesha mazingira yasiyokuwa ya haki.

Aidha walidai kuwa matokeo yalipotoka mgombea wa CCM alipunguziwa idadi ya kura zake jambo walilodai lilikuwa sio la haki pia.

Katika madai yao walalamikaji hao walizidi kudai kupitia mashahidi wao kuwa zoezi zima la kupiga kura na kutoa matokeo lilikiuka taratibu kama zinavyosimamiwa na Tume ya Uchaguzi (NEC).

Katika ushahidi uliowasilishwa katika mahakama hiyo walalamikaji walidai kuwa fomu za matokeo ya uchaguzi huo zilikuwa feki na kwamba zilitumika mahususi kumpa ushindi Dk. Slaa.

Akitoa hukumu hiyo iliyosomwa kwa muda wa masaa mawili, Jaji Robert Makaramba alisema kuwa hoja za walalamikaji hazina msingi wa kisheria wa kutengua matokeo hayo yaliyompa ushindi Dk. Slaa.

``Hoja zote zilizowalisilishwa mbele ya mahakama hii na walalamikaji haziwezi kubatilisha matokeo ya uchaguzi unaolalamikiwa`` alisema Jaji huyo wakati akisoma hukumu hiyo.

Akiendelea kuchambua hoja hizo, Jaji Makaramba alisema kuwa hoja za mgombea wa CCM hazina msingi kwani hata kama angeongezewa kura wanazodai kuwa alipunjwa zisingetosha kumpa mgombea huyo ushindi.

``Kutokana na ushahidi uliowasilishwa mbele ya mahakama hii na pande zote, hata mgombea wa CHADEMA naye alipunjwa na kama naye angeongezewa kura alizopunjwa basi angeendelea kuwa mshindi`` alisema Jaji Makaramba katika hukumu yake.

Mara baada ya Jaji kumaliza kusoma hukumu hiyo wanachama wa CHADEMA waliojaa katika viwanja vya mahakama hiyo walianza kupiga vigelele na kuimba nyimbo za furaha.

Baada ya hukumu hiyo, Dk. Slaa alisema kuwa alijua toka awali kuwa hakuna kesi ya maana iliyofunguliwa na walalamikaji dhidi yake na kwamba alitarajia kuwa angetendewa haki kama ilivyooneka.

Upande wa walalamikaji pamoja na mawakili wao walitoweka haraka mahakamani hapo mara baada ya hukumu hiyo kuisha na walipotafutwa hata kwa njia ya simu kutoa maoni yao hawakuweza kupatikana.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.