|
CUF, CCM rejeeni mezani - Kikwete
2008-05-16 10:20:16
Na Mwandishi Wetu
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, amekitaka Chama cha Wananchi (CUF), kurudi katika mazungumzo ya mwafaka na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema misimamo iliyotolewa na pande mbili, kiasi cha kuibua malumbano na kushutumiana, imedhihirisha kuwa tofauti iliyopo ni namna ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.
``Baada ya vyama CCM na CUF kuwa vimeweka misimamo yao kuhusu mwafaka, sasa ni wakati wa kurudi mezani kuendeleza majadiliano,`` alisema Rais Kikwete, alipokutana na wageni waliomtembelea kwa nyakati tofauti Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilimkariri Rais Kikwete akisema, anaamini kuwa majadiliano hayo hatimaye yatazaa matunda mazuri kwa mustakabali wa Tanzania.
Katika mazungumzo yake na Waziri wa Nchi wa Ufaransa anayeshughulikia mahusiano ya kimataifa na nchi zinazozungumza Kifaransa, Alain Joyandet, Rais Kikwete, alitumia muda mrefu kuelezea historia ya majadiliano ya mwafaka na sababu zilizopelekea kuanzishwa kwa majadiliano hayo.
``Naamini mambo yatakwenda vizuri, hatimaye tutafanikiwa katika hili la mazungumzo la mwafaka,`` alisema Rais Kikwete.
Alisema kimsingi, CCM na CUF vinakubaliana kuhusu mambo ya kufanyika juu ya mwafaka, na kuwa tofauti ni katika utekelezaji wa hayo yaliyokubaliwa.
CCM wanataka suala hilo kubwa la msingi liamuriwe moja kwa moja na wananchi. CUF wao wanataka wanasiasa kuamua kwa niaba ya wananchi. Hivyo, tofauti iko katika namna ya kutekeleza yaliyokubaliwa, alisema.
Rais Kikwete, alisema uamuzi wa kuwa na serikali shirikishi katika Zanzibar ulichukuliwa mwaka 2001, wakati wa majadiliano yaliyozaa mwafaka wa kwanza kati ya CCM na CUF.
Rais alisisitiza kuwa uamuzi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM katika kikao chake cha karibu cha Butiama, haukubadilisha makubaliano ya msingi kati ya vyama hivyo.
Kilichofanyika ni CCM kuongeza mapendekezo mawili ili nayo yajadiliwe na timu za vyama hivyo viwili.
Alisema pendekezo moja ni kuwashirikisha wananchi kuamua utekelezaji wa mwafaka kati ya vyama hivyo, na la pili ni kuweka utaratibu wa ukomo wa utekelezaji wa muafaka huo.
``Mwafaka unalenga kuitoa Zanzibar katika matatizo ya sasa ya kisiasa, hauwezi kuwa utaratibu wa daima dumu na kuwa ukifika wakati kuwa mfumo huo wa utawala wa kisiasa umekamilisha kazi yake, basi unaweza kuondolewa na Zanzibar ikarudi katika ushindani wa kawaida wa kisiasa`` alisema.
Alisema kuwa hivyo ndivyo ilivyokuwa katika nchi za Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Kenya.
Katika mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Kenya, Bw. Adam Woods, Rais Kikwete alisisitiza kuwa bado iko nafasi ya kuokoa mazungumzo hayo ya mwafaka.
``Wote sasa wamezungumza kiasi cha kutosha, sasa ni wakati wa kukaa chini na kuendelea na mazungumzo``alisema.
``Maamuzi ya CCM hayajabadilisha jambo lolote la msingi katika makubaliano ya mwafaka, no deviation on fundamental agreement.
Tulichofanya sisi ni kuongeza jambo la kuwashirikisha wananchi na kuwataka wanaoendesha majadiliano kulifikiria na hili,``alisema.
|