|
Wapemba si wahaini
2008-05-16 10:26:10
Na Simon Mhina
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani hatua ya Serikali kuwashikilia watu waliowasilisha waraka Umoja wa Mataifa wakitaka kisiwa cha Pemba kijitenge na kuwa huru.
Aidha kituo hicho kimesema kuwasilishwa kwa waraka huo UN sio uhaini kwa kuwa ni suala la maoni linakubalika kikatiba.
Akizungumza na Nipashe ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, mwanasheria wa kituo hicho, Bw. Clarence Kipobota, alisema kitendo cha watu hao kutoka Pemba kuandika waraka na kutoa madai hayo, hakikidhi haja ya wananchi hao kushtakiwa kwa kosa la uhaini.
Alisema hata hatua ya Serikali kuwashikilia watu hao kwa muda mrefu na kuwahifadhi sehemu isiyofahamika, huku ikiwakataza ndugu zao kuwaona, ni ushahidi mwingine kwamba imekosa vifungu vya sheria vya kuwashtaki.
Akifafanua, mwanasheria huyo alisema kwa mujibu wa Kanuni za Makosa ya Jinai, lazima ithibitike kuwepo na ‚kunuia uovu pamoja na kitendo kiovu.
``Mambo hayo yakithibitika ndipo kunazaliwa neo jinai`` alisema Bw. Kipobota.
Aidha alisema uhaini maana yake ni kutaka kuiondoa madarakani serikali halali iliyowekwa kwa mujibu wa Katiba kwa njia yoyote, ikiwa ni pamoja na kumuua Rais au kwa namna nyingine.
Alisema pia uhaini unaweza kutokana na mtu au kikundi kuanzisha vita vinavyoanzia ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano, kwa nia hiyo hiyo ya kuiondoa Serikali madarakani.
``Sasa tukitafakari kwa makini mambo haya mawili ya Jinai na Uhaini. Watu wale (waliokamatwa) wametafakari kwenye mioyo yao wakasema kwa vile wamebaguliwa siku nyingi na mwafaka kati ya CCM na CUF, ambao ulikuwa tumaini lao umetoweka, njia sahihi yenye manufaa kwao ni kujitenga.
Hiyo sio nia ovu kwa vile wametaka kufanya hivyo kwa utaratibu na kutumia njia zinazokubalika kikatiba’’ alisema.
``Baada ya kutafakari wakaamua kuandika barua na kuwasilisha maoni yao waziwazi bila kificho. Je, kufanya hivyo ni kitendo kiovu? Hapana, hakuna kitendo kiovu kilichofanyika, kwa hiyo hii sio jinai.``
Kuhusu uhaini, Bw. Kipobota alisema mahakama ilishatoa hukumu kwamba hakuna mtu anayeweza kuipindua Zanzibar kwa vile sio nchi, kwa maana ya kwamba haina dola kamili.
Alisema kwa mtu mwenye busara, atang`amua kwamba walichokifanya Wapemba hao, hata kama hakipendezi hawakuwa na nia mbaya, bali walikuwa wanatoa maoni yao.
Alisema ndio maana maombi hayo wameyaweka wazi, na kuyawasilisha kwenye chombo kinachoaminika duniani kote.
``Wanaposema waandishi wa barua hiyo ni wahaini, ina maana basi hata Umoja wa Mataifa, nao ni wahaini kwa vile wamekula njama na kupokea barua ya wahaini,alisema na kuongeza, hakuna uhaini unaoweza kufanyika kwa kutumia mtindo wa kistaarabu kiasi hiki.``
Alisema kwa vile kushirikiana na mhaini, moja kwa moja na wewe unaingia kwenye kundi hilo, kama kweli Serikali inashikilia msimamo wake wa kuwaita wananchi hao wahaini, haina budi kuwaunganisha kwenye kesi hiyo na maofisa wa UN.
Alisema kitendo cha kuandika barua hiyo hakiashirii kuiondoa Serikali madarakani, wala kumdhuru Rais.
``Walichokifanya wananchi hao hakitoshelezi kuitwa wahaini, wala hakina dalili zozote za jinai zaidi ya kutoa mawazo yao,`` alisema Bw. Kipobota.
Kuhusu watuhumiwa hao kushikiliwa kusikojulikana, Mwanasheria huyo alisema Serikali inafanya makosa makubwa na inakiuka haki za msingi za binadamu.
Vile vile alisema kitendo hicho cha Serikali, ni uvunjaji wa sheria za nchi, ambazo inategemewa kuzilinda na kuzisimamia.
Alisema kwa mujibu wa sheria kuna sehemu mbili tu, ambapo dola inaweza kushikilia mtuhumiwa.
Alisema sehemu ya kwanza ni mahabusu zilizopo polisi na kwenye magereza, ili mradi wasichanganywe na watu ambao tayari wamehukumiwa.
``Sasa tunapoelezwa kwamba haijulikani wanashikiliwa wapi, moja kwa moja kushikiliwa kwao ni batili, kwa vile hawapo polisi wala magerezani,`` alisema.
Bw. Kipobota alisema kitendo cha kuzuia watuhumiwa hao kuonana na jamaa zao, pia ni uvunjaji wa sheria na haki za msingi za binadamu.
Alisema kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa anayo haki ya kuonana na ndugu na kuwaeleza kwamba amekamatwa, na kuambiwa anapelekwa wapi.
Pia mtuhumiwa anayo haki ya kuwakilishwa kortini, hivyo apewe fursa ya kukutana na wakili wake na kufikishwa mahakamani mapema iwezekanavyo, badala ya kusota kusikojulikana kama Wapemba hao.
``Kwa hiyo Kituo cha Sheria za haki za Binadamu kinaitaka Serikali kuwaachia wananchi hao au iwafikishe mahakamani,``alisema.
|