17 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Stars ifanye kweli Kampala
 
2008-05-17 08:53:57
Na Mhariri

Timu ya soka ya taifa, Taifa Stars leoinaivaa timu ya Uganda, The Cranes katika mchezo wa marudiano wa mtoano ya michuano ya Afrika inayoshirikisha wanasoka wanaocheza ligi za ndani.

Mchezo huo unatazamiwa kuchezwa katika uwanja wa Nakivubo mjini Kampala, Uganda.

Stars inaingia katika mchezo huu ikiwa na nafasi nzuri baada ya kuiliza Uganda 2-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa mjini Mwanza.

Kwa matokeo hayo sasa, Stars inahitaji sare au kufungwa chini ya mabao mawili na kuweza kusonga mbele katika michuano hiyo.

Uganda nayo inatakiwa kupata ushindi wa 3-0 au angalau kushinda 2-0 ili kuweza kupata fursa ya kupigiana penati.

Mchezo huu unatazamiwa kuwa na presha kubwa pia kwa makocha wa timu zote mbili.

Kocha wa Stars, Mbrazil Marcio Maximo amekuwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha anainua kiwango cha Stars.

Watanzania baada ya kukosakosa kufuzu kwa fainali za Kombe la mataifa ya Afrika zilizofanyika mwaka huu nchini Ghana, sasa wanataka kuona timu hii inafanya vizuri katika mashindano haya.

Waganda nao wamekuwa wakimpa wakati mgumu kutoka kocha wao, Lazlo Szabo kutoka Hungary na kufanya hali ya mchezo wa leo kuwa mgumu.

Watanzania wataingia katika mchezo huu wakiwa na matumaini makubwa kutokana na Maximo kuonekana kuanza kupata kikosi cha kufanya vizuri katika siku za usoni.

Kiungo Mrisho Ngassa, washambuliaji Jerr Tegete na Uhuru Selemani na beki Narib Haroub `Cannavaro` wanatoa matumaini makubwa ya timu hiyo kufanya vizuiri katika mchezo huo.

Yosso hao, ambao wataongezwa nguvu na wakongwe kama kipa, Ivo Mapunda na Emmanuel Gabriel wanatoa moyo kwa Stars kuweza kusonga mbele.

Pia timu zote mbili zitakuwa na njaa ya mafanikio ya kuweza kufuzu kwa fainali za michuano mikubwa ya Afrika.

Uganda imefuzu mara moja tu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nayo ilikuwa mwaka 1978 wakati fainali zilipofanyika nchini Ghana.

Nayo Stars ilifuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 wakati zilipofanyika nchini Nigeria.

Bila ya shaka leo, Maximo atakuwa amewandaa wachezaji vizuri ili kuweza kuwang'oa Waganda.

Ni kweli Waganda watakuwa nyumbani na bila shaka wakatumia kila mbinu kushinda lakini vizuri vijana wa Stars wakazingatia mafunzo ya kocha wao na kufanya kweli.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.