14 Aug 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Sekta ya utalii na mchango wa kupunguza umaskini
 
2008-08-14 11:49:56
Na Theo Mushi

Sekta ya Utalii imekuwa mojawapo ya sekta za kiuchumi zinazokua haraka sana nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na sekta za madini na ujenzi.

Hii ni kwa sababu katika miaka kumi na zaidi iliyopita wawekezaji wa nje na ndani ya nchi wamewekeza sana katika sekta ya utalii kwa ujenzi wa mahoteli, kuanzisha makampuni ya kusafirisha watalii pamoja na uwekezaji mwingine uliochochea ukuaji wa sekta hii.

Pamoja na hayo yote, sekta ya utalii na madini ambazo zilipata wawekezaji wengi, hazijachangia sana katika juhudi za kupunguza umaskini kwa sababu hazikuzi ajira au nafasi nyingi za mapato kwa wananchi wengi kama zilivyo sekta za kilimo na viwanda.

Mwaka 2007 Tanzania ilipata watalii 719,031 waliotembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini na nchi ilifaidika kupata fedha za kigeni zinazokaribia dola milioni 800 za Kimarekani.

Sekta ya Utalii imekuwa kwa asilimia 12 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na mchango wake katika pato la taifa ni asilimia 17.2 na mapato ya fedha za kigeni ni asilimia 25 ya mapato yote ya kigeni yanayotokana na kuuza bidhaa za huduma mbalimbali nje ya nchi ikiwemo huduma ya utalii.

Kukua kwa sekta ya utalii kumetokana na juhudi kubwa iliyofanywa na Bodi ya Utalii (Tanzania Tourist Board) katika kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii nchini na nje ya nchi.

Inatarajiwa kwamba ifikapo mwaka 2010 idadi ya watalii watakaowasili nchini itafikia milioni moja na mapato yatokanayo na utalii yatafikia dola bilioni moja za Kimarekani.

Hii inaonyesha kwamba sera na mipango kamambe ya kuendeleza sekta ya utalii imetekelezwa kama ilivyopangwa na kupata mafanikio hayo.

Kumekuwa na mkazo katika kuendesha utalii endelevu unaokubalika kijamii ukizingatia utunzaji mazingira, uchumi, kukuza na kuhifadhi utamaduni wa Watanzania.

Kumekuwa na mpango maalum uliofadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya (European Union) wa kutoa mafunzo kwa wote wanaotoa huduma kwa watalii ili kuboresha kiwango cha huduma hiyo .

Jinsi watalii wanavyopokelewa vizuri na ukarimu unaoonyeshwa watalii watasifia nchi ya Tanzania na kuwashawishi wengine waje kutembelea nchi hiyo na vingine kurudi mara nyingine na kukaa muda mrefu zaidi.

Mafunzo hayo yalilenga zaidi kwa wahudumu wa mapokezi, huduma za vinywaji na vyakula, wahudumu wa vyumba pamoja na wapishi.

Malengo yalikuwa ni kuwafunza watumishi wa mahoteli, mawakala wa utalii, wasafirishaji pamoja na wabeba mizigo njia bora ya kutoa huduma ya hali ya juu zaidi kwa watalii.

Waliofaidika na mipango hiyo ya mafunzo ni pamoja na Chuo cha Taifa cha Utalii tawi la Dar es Salaam na Arusha, Njuweni (Pwani), Masoka (Kilimanjaro), Chuo cha Utalii Zanzibar na Chuo cha VETA Mikumi, Morogoro.

Matokeo yake ni kuboresha huduma za mahoteli kwa watalii na huduma zote zinazohitajika na watalii zikiwepo za usafiri, mapokezi viwanja vya ndege na kukarimu watalii kwa ujumla.

Ukuaji wa sekta ya utalii unaenda sambamba na kuongezeka kwa makampuni yanayohusika na biashara ya utalii. Hivyo mapato yatokanayo na leseni mbalimbali yalifikia Sh. 1.8 bilioni (2007) ambazo zinahitajika kutumiwa kuboresha miundombinu kama vile barabara zinazoelekea kwenye mbuga za wanyama.

Zaidi ya kuwa na vivutio vingi ili idadi ya watalii iongezeke nchi ni lazima iwe na amani, umoja na utulivu, mshikamano na utamaduni kwa kupenda na kukaribisha wageni.

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imefanya kazi nzuri katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania na katika nchi mbalimbali kama vile Canada, Marekani, Uingereza na Jumuiya ya Ulaya. Imejaribu kuzishirikisha ofisi za mabalozi wa Tanzania nje ya nchi ili kutangaza biashara ya utalii katika enzi hizi za diplomasia ya kiuchumi (economic diplomacy) ambayo mkazo ni biashara, uwekezaji na utalii.

Kwa kutumia mikakati mbali mbali TTB imetangaza nchi za nje vivutio vya asili kama Mlima Kilimanjaro, hifadhi ya wanyama ya Gombe, Katavi, Mkomazi, Serengeti, Ngorongoro Crater na mbuga za Selous.

TTB imetangaza vivutio vya kitalii kutumia CNN International ya Marekani ambayo ni televisheni yenye watazamaji zaidi ya milioni 152. Mabango yaliwekwa katika mabasi ya abiria 124 na katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Heathrow (London) kwa kipindi cha miezi mitatu na kutazamwa na zaidi ya watu milioni kumi walioonyeshwa ramani ya Tanzania na vivutio vya utalii vya nchi hii.

Zaidi ya mawakala wa utalii 1800 wa Marekani na Canada walipewa mafunzo kuhusu biashara ya utalii Tanzania na mambo mengine yalitangazwa katika USA Travel Agent Journal.

Tanzania iliweza kushiriki katika maonyesho ya 22 ya biashara ya utalii ili kutangaza vivutio vya utalii.

Imebainika kwamba vivutio vya utalii peke yake haviwezi kukuza biashara ya utalii na kuwafanya watalii waje na kukaa muda mrefu na kutumia fedha zao kununua bidhaa na huduma mbali mbali zinazotolewa nchini.

Kuna umuhimu wa kuendeleza utamaduni ili uvutie watalii na hivi sasa vikundi 24 vya utamaduni vimeundwa kutoa burudani kwa watalii katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Pwani, Tanga na Mbeya.

Vivutio, ukarimu na kutangaza vivutio vya utalii ni lazima viendane na kuongeza bidhaa na huduma mbali mbali za utalii.

Mikakati inayotakiwa kuzingatiwa ni pamoja na kukuza utalii wa mijini (Urban tourism) kwa kujenga mahoteli yenye huduma za vilabu vya usiku (night clubs) pamoja na casino.

Kuna umuhimu wa kuhifadhi urithi wa kihistoria kama vile majengo ya Wajerumani Bagamoyo, Lushoto, Dar es Salaam na miji mingine.

Vile vile kuna majengo ya kihistoria ya ujenzi wa Kiarabu Zanzibar `Stone Town` ambayo yanavutia watalii.
Katika kipindi ambacho hakina watalii wengi wa nje ya nchi kuna umuhimu wa kutoa motisha kwa watalii wa ndani ya nchi ili watembelee mbuga za wanyama kama vile Mikumi.

Makundi yatakayolengwa ni wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo vya elimu ya juu pamoja na wafanyabiashara.

Hakuna uhakika kwamba kukua kwa sekta ya utalii na mchango wake katika uchumi wa taifa vimechangia katika juhudi na mikakati ya kupunguza umaskini.

Wakati wa kujenga mahoteli vibarua na mafundi hupata ajira ya muda na vile vile katika kujenga barabara zinazoingia katika mbuga za wanyama.

Lakini baada ya ujenzi huu katika ngazi za kati za utawala na nagazi za juu watumishi wengi hutoka nje ya nchi na katika ngazi za chini ndiyo utakuta Watanzania kama mabawabu na walinzi (korokoroni).

Kutakuwa na mchango katika kupunguza umaskini kama hoteli hizi zikinunua mahitaji yao hapa nchini kama vyakula, samani na bidhaa mbalimbali kutoka soko la ndani ya nchi.

Hii itaongeza ajira na kipato na hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini. Kuna sababu gani ya kutonunua nyama ya ranchi ya Kongwa na kuagiza nyama Afrika ya Kusini na Botswana? Au kuagiza `apples\' kutoka Los Angeles Califonia wakati kuna matunda hayo Lushoto mkoa wa Tanga?

Watali hununua bidhaa za kiutamaduni kama vinyago vya kimakonde, shanga za kimasai na nguo za batiki zilizodariziwa na Watanzania.

Na hii husaidia kuongeza mapato na ajira katika viwanda na biashara ndogo na za kati (SMEs). Kuna mambo ambayo kama hayatatazamwa yataathiri utalii na hayo ni pamoja na kulinda amani, utulivu na kutokuwa na migogoro ya kisiasa.

Mambo mengine ni kupiga vita ujambazi, utapeli pamoja na uhalifu kwa ujumla.

Kuna umuhimu wa kushirikiana na nchi nyingine kupiga vita ugaidi ili nchi za magharibi zisianze kutoa onyo kwamba raia wake hawatakuwa salama wakitembelea nchi za Afrika ya Mashariki.

Uharibifu wa mazingira na hasa fukwe za baharini utapunguza vivutio vya utalii na hasa bahari, jua na fukwe. Kuongezeka kwa hali ya joto duniani kunatishia kutoweka kwa theluji juu ya Mlima Kilimanjaro ambacho ni kivutio kikubwa cha utalii.

Ili utalii uwe na manufaa kwa nchi na watu wake huduma za shule, zahanati na barabara ni lazima vijengwe kwa jumuiya zinazoishi karibu na mbuga za wanyama kama Manyara, Ngorongoro na Serengeti.

Hawa wanatakiwa kuwa watu wa kwanza kunufaika na utalii kwa sababu wataendelea kutoa ushirikiano katika kuhifadhi vivutio vya utalii ikiwa ni pamoja na wanyama pori wanaopatikana katika mbuga za taifa.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.