21 Aug 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mikoa ya kusini kunufaika na teknolojia ya kilimo cha mazao mbadala
 
2008-08-21 09:04:41
Na MORIS LYIMO

Yawezekana miundo mbinu ilichelewesha maendeleo ya Mikoa ya Kanda ya Kusini. Hata tulipoona mabadiliko ya hali hiyo, bado uchumi wa mikoa hiyo unaotegemea kilimo bado ulidorora.

Kituo cha utafiti Naliendele cha mkoani Mtwara kilibaini udhaifu huo, kutafiti teknolojia endelevu za kilimo cha mazao mbadala kama karanga na ufuta.

Utafiti katika masoko ya ndani na nje kwa mazao yatokayo Tanzania unaonyesha kuwa mazao ya ufuta na karanga yana bei kubwa katika mzunguko wa masoko duniani na kuzidi mara dufu ya mazao mengine ya asili kama kahawa, pamba na korosho.

Hata hivyo , mazao hayo yamekosa kujulikana vyema sokoni kwa kukosa kuendelezwa, kutangazwa na changamoto nyingine kama vile wakulima kutopata fedha za programu ya kuendeleza sekta ya kilimo (ASDP) kupitia programu kama hiyo wilayani (DADPs).

Karanga ni zao jamii ya mikunde ambalo asili yake ni Amerika ya Kusini, liliingizwa barani Afrika upande wa magharibi na Wareno kutoka Brazili kwenye karne ya 16.

Hata hivyo ukulima wa zao hilo katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukisuasua kutokana na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni mitaji midogo ya wakulima, ardhi kukosa rutuba, na ukosefu wa mbegu bora.

Kilimo cha karanga katika mikoa ya kusini kimeanza kuleta mafanikio makubwa kwa wakulima wadogo baada ya wakulima hao kuwezeshwa kushirikishwa katika teknolojia za utafiti wa mbegu bora za karanga ambazo matokeo yake yameanza kukomboa familia masikini vijijini kwa vile ni zao ambalo halihitaji nguvu kubwa, pembejeo kwa maana ya mbolea na madawa ya kudhibiti viuatilifu.

Maeneo ambayo yamefaidika na mpango huo ni wilaya ya Ruangwa, Nachingwea (Lindi), Nanyumbu na Masasi kwa mkoa wa Mtwara.

Mratibu mtafiti wa kituo cha utafiti na mafunzo Niendele kupitia mradi wa uendelezaji wa mazao ya mikunde.

Dk. Omari Mponda anasema fursa ya kulitumia zao la karanga katika kuondoa umaskini wa kipato na lishe bado haijatumika ipasavyo.

Hii ni kutokana na uzalishaji wa karanga kwa eneo hilo nchini bado ni mdogo licha ya kuwepo kwa kanuni za kilimo bora cha zao hilo ambalo pia ni muhimu kwa kutoa nitrojeni kwenye ardhi mashambani hivyo kufanya rutuba ya udongo kuongezeka na kulinda mazingira.

Katika maeneo mengi yaliyotembelewa, kwa wastani mkulima huvuna kiasi cha kilo 600 kwa hekta, ingawa Dk. Mponda anasema utafiti umeonyesha kwa kutumia kanuni za kilimo bora cha karanga mkulima anaweza kuvuna zaidi ya kilo 1,500 kwa hekta za karanga zilizobanguliwa.

Hata hivyo Dk. Shamte Shomari ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya ARI - Naliendele kanda ya kusini anasema ongezeko la uzalishaji wa zao la karanga unakwamishwa na wakulima wengi kuendelea kutumia mbegu duni kutokana na uhaba wa mbegu bora zilizothibitishwa, ukosefu wa mbegu bora kulingana na mahitaji ya soko, ukame, magonjwa na mashambulizi mengine kama vile wadudu waharibifu.

Matatizo mengine ni ukosefu wa mpangilio juu ya usimamizi wa uzalishaji na ununuzi wa zao la karanga, mfumo wa ununuzi kutawaliwa na ubabaishaji kwa maana wafanyabishara wachache kuendelea kuwalaghai wakulima kuuza karanga zao kwa bei ya chini.

Kuondokana na yote hayo Dk. Shomari anasema ARI-Naliendele imekusudia kutoishia katika utafiti pekee, pia kuwaunganisha wakulima na maofisa ugani vijijini kwa kuwapa miongozo kuhusu jinsi ya kuzalisha mbegu bora hatua kwa hatua katika maeneo yao hivyo kufikia malengo ya kuwa na kilimo cha kisayansi na endelevu.

Aina ya mbegu bora zilizopatikana hapa nchini ni Nyota, Johari, Sawia na Pendo, ambapo utafiti wa mbegu bora zaidi unaendelea katika kituo cha utafiti na mafunzo Naliendele kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Utafiti na Uendelezaji wa Mazao yanayostahimili Ukame (ICRISAT).

Dk. Mponda anasema, lengo ni kupata mbegu zinazokidhi mahitaji ya soko na wakulima, zinazovumilia ukame, magonjwa na wadudu.

Kufuatana na utafiti shirikishi uliofanyika, aina mpya za mbegu bora zimeweza kutambuliwa na zipo katika hatua ya mwisho kutolewa kwa wakulima.

Aina mojawapo ya mbegu bora mpya ni Mnanje 2007 ambayo tayari imeanza kuenea katika Mkoa wa Mtwara hasa Wilaya ya Masasi na Nanyumbu.

Dk. Mponda anasema kutokana na mpango wao shirikishi wa wakulima na maofisa ugani wakulima, katika maeneo ya Mnanje, Likokona na Mpeta wameweza kuzalisha tani 140 katika msimu huuu, ambapo ARI - Naliendele wamenunua tani saba zitakazosambazwa kama mbegu kwa wakulima msimu ujao.

``Tuna nia nzuri ya kuongezea wakulima uzalishaji, tija.
Changamoto tuliyonayo ni namna ya kuwafikia wakulima wote na kuwajengea uwezo ili kufikia lengo la matarajio ambayo ni kuzalisha mara dufu, kupitia njia ya makundi ya wakulima, mashamba darasa,`` anasema Dk. Mponda.

Anasema, wakulima wengi wanahitaji elimu kuanzia kuibua miradi , kwa ufanisi, mafunzo na mbinu bora za kilimo, ambapo kupitia fedha za DADPs wanaweza kujengewa uwezo.

Uchunguzi unaonyesha kuwa wakulima wengi vijijini hasa maeneo ambayo wakulima wameonyesha nia ya kujiunga na kuanzisha mradi wa kilimo cha karanga, na shamba la mfano hawafaidiki na fedha za serikali zinazotolewa kupitia programu ya ASDP kwenda halmashauri za wilaya.

Kutokana na hali hiyo, hakuna uhakika wa wakulima kujengewa mazingira ya kuwa na utamaduni wa kutunza mbegu, jukumu ambalo wakala wa mbegu chini ya Wizara ya Kilimo anapaswa kujua na kupatikana kwa suluhisho la tatizo la mbegu na kuwahakikishia wakulima upatikanaji wa mbegu.

``Tunapozungumzia `mapinduzi ya kijani` yaani kitaalamu (green revolution) lazima tuangalie lengo la serikali ambalo ni kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa sasa wa kilo 600 - 700 na kufikia kilo 1,200 kwa ekari moja yaani kutoka nusu tani hadi zaidi ya tani moja kwa ekari,`` anasema.

Kwa hiyo mtafiti huyo anasema mapinduzi hayo yanaweza kufikiwa kwa kuwajengea wakulima uwezo, miundo-mbinu, uhakika wa mbegu na pembejeo muhimu, anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Bw. Aseri Msangi anasema wakulima wengi wa wilaya yake wamefaidika na mafunzo ya kilimo cha kisasa cha karanga yanayotolewa na kituo cha utafiti cha mafunzo ARI-Naliendele tangu wilaya hiyo ilipoanzishwa rasmi mwaka 2006.

DC Msangi anasema tatizo kubwa linalokwamisha uzalishaji ni fedha za serikali za kuendeleza kilimo (ASDP) kutofika wakati wa msimu wa kilimo.

Anasema yeye amepita kila kijiji kuhamasisha kilimo cha karanga aina ya Pendo zinazostawi zaidi katika wilaya yake na kuwahamasisha wakulima waache kulima karanga za kienyeji, na kuacha uvivu.

``Tumetafiti na kuona karanga za Pendo zinakubalika vizuri katika soko, zinahimili magonjwa, na zinachukua muda mfupi (siku 90) tangu kupandwa hadi kuvunwa, lakini fedha hazifiki wakati muafaka,`` anasema Bw. Msangi.

Katika msimu wa mwaka huu wilaya ilivuna tani 5,000 za karanga na mpango ni kuongeza uzalishaji kufikia tani 12,000 na kufanya uchumi/pato la mkulima kuongezeka ingawa vifaa vya kukaushia, kubangua na elimu/uelewa mdogo miongoni mwa wakulima ni kikwazo.

Kuhusu soko, anasema nguvu ya pamoja ya mkoa mzima inahitajika. Kwani anasema kutokana na kasumba ya miongoni mwa wafanyabiashara kuendelea kuwarubuni wakulima, hivyo anashauri mazao yote yaingizwe katika mfumo wa stakabadhi ghalani kama malipo hayo yanavyofanywa kwenye zao la korosho mkoani Mtwara.

Pia uelewa mdogo wa waendeshaji wa vyama vya msingi kutokana na kuendelea bei zisizofanyiwa tathimini ya gharama za uzalishaji na wakulima kutofahamu umuhimu wa kuuza katika vyama vya msingi vya kijiji.

DC Msangi anasema ipo haja ya kuwa na vikundi vingi vya wakulima vya uzalishaji wa mbegu kupitia DADPs, PADEP vitakavyopewa uwezo wa uzalishaji na kuwa na uhakika wa mbegu.

Naye Mkuuwa wa Wilaya ya Masasi Bw. Saidi Amanzi amesema wilaya yake imejiwekea mkakati wa kulima mazao mchanganyiko kama karanga, ufuta na mbaazi kwa kitaalamu zaidi.

``Haya ni maagizo ya mkoa hivyo lazima tuyatekeleze ili kuwa na ukulima wenye tija. Mazao yote, isipokuwa mbaazi yatalimwa katika mashamba ya mikorosho iliyokatwa matawi pembeni kupisha ustawi mzuri wa karanga na ufuta,`` anasema DC Amanzi.

Pia kulima mazao ya matunda, migomba, kwa njia ya kisasa na ufugaji wa kisasa, na kila familia kuwa na ekari nne za karanga, ufuta na mazao mengine ambapo wakulima wengi wanaendelea kuelimishwa.

Amesifu jitihada zinazofanywa na ARI - Naliendele na kushauri fedha za ASDP kuwafikia wakulima mapema. Tayari baadhi ya vikundi vya wakulima wa karanga vimeanzishwa huko Mpeta na Likokona ambavyo vimepiga hatua kubwa kwa uzalishaji.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.